IJUMAA JUMA 22 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kol.1:15-20
Kristo Yesu ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika
yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana;
ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na
kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye
kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba
awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye
kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye,
ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.100:2-5 (K)2
1. Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba;
(K) Njoni mbele ya Bwana kwa kuimba kwa furaha.
2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
3. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake; (K)
4. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)
SHANGILIO: Lk.5:33-39
Aleluya, aleluya!
Je, wale walioalikwa harusini
hutakiwa wafunge hali bwana arusi yuko pamoja nao?
Aleluya!
INJILI: Lk.5:33-39
Mafarisayo na waandishi walimwambia Yesu, Wanafunzi wa Yohane hufunga mara nyingi, na kuomba
dua; na kadhalika wanafunzi wa Mafarisayo; lakini wanafunzi wako hula na kunywa! Lakini Yesu
akawaambia, Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo bwana arusi pamoja nao?
Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku zile. Akawaambia
na mithali, Hakuna akataye kiraka cha vazi jipya na kukitia katika vazi kuukuu; na kama akitia,
amelikata lile jipya, na kile kiraka cha vazi jipya hakilingani na lile vazi kuukuu. Wala hakuna
mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama akitia, ile divai mpya itavipasua vile
viriba, divai yenyewe itamwagika, na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya sharti kutiwa katika
viriba vipya. Wala hakuna anywaye divai ya kale akatamani divai mpya; kwa kuwa asema, Ile ya
kale ndiyo iliyo njema.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu ambaye pamoja na Mwanae,
Yesu Kristo, anautawala kabisa ulimwengu huu mpya:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Baba Mtakatifu wetu F., kumwakilisha
kiaminifu Kristo Mwanao, aliye kichwa cha Kanisa,
ili watu wako watubu na kupata wokovu. Ee Bwana.
2. Upende kuwakumbusha daima watawala wa dunia
kuwa vitu vyote viliumbwa kwa njia ya Kristo na kwa
ajili yake. Ee Bwana.
3. Kwa njia ya amani ambayo Mwanao Yesu Kristo
alifanya kwa damu yake msalabani, utujalie utimilifu
wote na kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake. Ee Bwana.
4. Utujalie kujiandaa vema kwa siku ya hukumu,
ambapo ya giza yatamulikwa, mashauri ya moyo
yatadhihirishwa na kila mtu atapata sifa yake kwako. Ee Bwana.
5. Kwa mastahili ya mateso, kifo na ufufuko wa
Mwanao Yesu Kristo, marehemu wetu wapewe uzima wa milele
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, unayetaka tufunge wakati wa kufaa kwa
wokovu wetu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.