IJUMAA JUMA 20 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Rut.1:1,3-6,14-16,22
Ikawa zamani za Waamuzi walipoamua, kulikuwa na njaa katika nchi. Akaondoka mtu mmoja wa Bethlehemu ya Yuda, akaenda kukaa katika nchi ya Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili. Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthuu. Wakakaa huko yapata miaka kumi. Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba Bwana amewajilia watu wake na kuwapa chakula. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthuu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. Naye Ruthuu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Basi Naomi akarudi; pamoja na Ruthuu Mmoabi, mkwewe; ambao walirudi kutoka nchi ya Moabu; nao wakafika Bethlehemu mwanzo wa mavuno ya shayiri.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.146:5-10 (K)2
1. Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, Na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake, Aliyezifanya mbingu na nchi, Bahari na vitu vyote vilivyomo.

(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.

2. Huishika kweli milele, Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula; Bwana hufungua waliofungwa; (K)

3. Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama; Bwana huwapenda wenye haki; Bwana huwahifadhi wageni; (K)

4. Huwategemeza yatima na mjane; Bali njia ya wasio haki huipotosha. Bwana atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. Haleluya. (K)

SHANGILIO: zab.27:11
Aleluya, aleluya!
Unifundishe njia yako, ee Bwana;
uniongoze katika njia iliyo sawa,
kwa sababu ya maadui zangu.
Aleluya!

INJILI: Mt.22:34-40
Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu uliyewafanya hata watu wa mataifa mengine, nje ya Israeli, wawe mfano katika kuitimiza Amri Kuu ya mapendo, twakuomba:-

Kiitikio: Usikie sala yetu.
1. Uwajalie Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu na Wakleri roho ya upendo usio na mipaka, wapate kuwavutia watu wengi kwako. Ee Bwana.

2. Uwajalie watu wa mataifa yote ukarimu kwa wenye njaa, wakimbizi, wageni na wote wenye matatizo mbalimbali. Ee Bwana.

3. Utujalie sisi sote kuyapokea na kuyatatua matatizo yetu kwa jicho la imani, na hivi kukutegemea siku zote na katika mazingira yoyote. Ee Bwana.

4. Utuimarishe katika imani ya ufufuko; na katika uwezo wako wa kuyatimiza yote uliyotuahidi na tunayoyahitaji kutoka kwako. Ee Bwana.

5. Uwape msamaha wa dhambi na kuwajalia uzima wa milele ndugu zetu marehemu. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyetupenda kiasi cha kumtoa Mwanao Yesu Kristo afe msalabani kwa ajili yetu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.