IJUMAA JUMA 18 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kum.4:32-40
Musa aliwaambia makutano: Uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu
aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya mbingu hata pemhe hii, kwamba kumetukia neno
lo lote kama neno hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili? Je! watu wakati wo
wote wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife? Au Mungu
amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara,
na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu,
kama vile Bwana, Mungu wenu, alivyowatendea ninvi katika Misri, mbele ya macho yenu? Wewe
umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa Bwana ndiye Mungu, hapana mwingine ila yeye. Kutoka
mbinguni amekusikizisha sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonyesha moto wake mkuu;
ukasikia maneno yake toka kati ya moto. Na kwa sababu aliwapenda baba zenu, kwa sababu hiyo
aliwachagua wazao wao baada yao, akakutoa katika Misri kwa kuwako pamoja nawe, kwa uweza wake
mwingi, ili kufukuza mbele yako mataifa, walio wakubwa, wenye nguvu kukupita wewe, ili kukuingiza,
na kukupa nehi yao iwe urithi, kama ilivyo leo. Kwa hivo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya
kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine. Basi, zishike
sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako,
na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.77:11-15,20 (K)11
1. Nitayakumbuka matendo ya Bwana,
Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale.
Pia nitaitafakari kazi yako yote;
Nitaziwaza habari za matendo yako.
(K) Ninayakumbuka matendo ya Bwana.
2. Ee Mungu, njia yako i katika utakatifu;
Ni nani aliye mungu mkuu kama Mungu?
Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu;
Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa. (K)
3. Kwa mkono wako umewakomboa watu wako,
Wana wa Yakobo na Yusufu.
Uliwaongoza watu wako kama kundi,
Kwa mkono wa Musa na Haruni. (K)
SHANGILIO: Mt.4:4
Aleluya, aleluya,
Mtu hataishi kwa mkate tu,
ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Aleluya.
INJILI: Mt.16:24-28
Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe,
ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu
atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu
wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? Kwa sababu Mwana
wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu
kwa kadiri ya matendo yake. Amin, nawaambieni, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao
hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, mafanikio katika kizazi hiki na kijacho
yatategemea uaminifu wetu katika kuzishika amri za
Mungu. Ili tuweze kufanikiwa katika hilo, tunahitaji
msaada wa Mungu. Tumwombe tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwajalie Baba Mtakatifu F., Maaskofu na Mapadre
tamaa ya kuwa karibu zaidi nawe katika sala, ili
wajaliwe zaidi na zaidi hekima ya kuliongoza Kanisa
lako. Ee Bwana.
2. Mataifa yote na yajue kuwa Wewe ndiwe Mungu
katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana
mwingine, ila Wewe. Ee Bwana.
3. Umjalie kila mmoja wetu kuitikia wito wa ufuasi
kwa kujikana mwenyewe, kujitwika msalaba wake
na kumfuata Mwanao Yesu Kristo. Ee Bwana.
4. Uwahurumie wote wanaoteseka na kudhulumiwa;
uwaokoe katika taabu zao na kuwajalia haki na amani. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapokelewe katika ufalme wako
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tuuthamini zaidi usalama wa nafsi
zetu kuliko kitu chochote, uyapokee maombi yetu. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.