IJUMAA JUMA 17 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Law.23:1,4-11,15-16,27,34-37
Bwana alinena na Musa, na kumwambia: Sikukuu za Bwana ni hizi, ni makusanviko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya Bwana. Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa Bwana ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba. Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. Lakini mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu; naye atautikisa mganda mbele za Bwana ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya sabato kuhani atautikisa. Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia sabato saba; hata siku ya pili ya hiyo sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka ya unga mpya. Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa Bwana. Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. Mtamsongezea Bwana sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. Sikukuu za Bwana ni hizi, ambazo mtazipigia mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee Bwana sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu, na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.8:2-5,9-10 (K)1
1. Pazeni zaburi, pigeni matari, Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda. Pigeni panda mwandamo wa mwezi, Wakati wa mbalamwezi, sikukuu yetu.

(K) Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha.

2. Kwa maana ni sheria kwa Israeli, Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo. Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu, Alipoondoka juu ya nchi ya Misri; Maneno yake nisiycmjua naliyasikia. (K)

3. Usiwe na mungu mgeni ndani yako; Wala usimsujudie mungu mwingine. Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza. (K)

SHANGILIO: 1The.2:13
Aleluya, aleluya!
Lipokeeni neno la Mungu,
siyo kama neno la wanadamu,
bali kama neno la Mungu.
Aleluya!

INJILI: Mt.13:54-58
Yesu alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.


--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa Ubatizo, sisi sote tumetunukiwa ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo, ili tumtumikie Mungu wetu. Kwa vile utume wetu unahitaji msaada wa Mungu, tumwombe.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Askofu wetu F. na mapadre wetu wote wajaliwe uvumilivu katika magumu wanayoyapata katika kazi zao za kitume. Ee Bwana.

2. Serikali zote ziwaruhusu watu wako kukuabudu Wewe kwa uhuru na amani. Ee Bwana.

3. Utujalie kushika kiaminifu sheria za Kanisa na kanuni zote za Liturjia na ibada mbalimbali, ili yote yaende kadiri ya mapenzi yako. Ee Bwana.

4. Kwa namna ya pekee tunawaombea wahubiri wa neno lako, ili wasiogope kuyakemea maovu yanayotendeka katika jamii, na uwape nguvu ya kustahimili upinzani wa waovu. Ee Bwana.

5. Uwakusanye kwako ndugu zetu marehemu wapate kuishi na kutawala nawe milele. Ee Bwana.

Ee Mungu uliye asili ya hekima na ufahamu wote, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.