IJUMAA JUMA 15 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.11:10-12:14
Musa na Haruni walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu,
asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake. Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri,
akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu.
Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwanakondoo,
kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwanakondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni
wachache kwa mwanakondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwanakondoo
mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu
yenu kwa yule mwanakondoo. Mwanakondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika
kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote
la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kutia katika miimo
miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule
ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile
mbichi wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama
zake za ndani. Wala msisaze kitu chake chochote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi
mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni,
na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana. Maana nitapita kati ya
nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu
na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. Na ile damu
itakuwa ishara kwenu katika ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lolote likawaharibu,
nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa
Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.116:12-13,15-18 (K)13
1. Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kulitangaza jina la Bwana.
(K) Nitakipokea kikombe cha wokovu,
na kulitangaza jina la Bwana.
2. Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Umevifunga vifungo vyangu. (K)
3. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana;
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote. (K)
SHANGILIO: Zab.119:28,33
Aleluya, aleluya!
Unitie nguvu sawasawa na neno lako,
ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya!
INJILI: Mt.12:1-8
Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza
kuvunja masuke, wakala. Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya
neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa
na njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho,
ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika
torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni,
kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema,
wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Yesu Kristo aliyetwaa mwili wetu wa kibinadamu
ni Mwanakondoo wa Pasaka, aliyetolewa kati yetu na
kuchinjwa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu wengi.
Na tumwombe.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Maaskofu na Mapadre wetu wazidi kutolea mara kwa
mara Sadaka ya Misa Takatifu kwa ajili ya
wokovu wa watu wako, wazima na wafu. Ee Bwana.
2. Uwaepushe watawala wa dunia na maasi yanayoweza
kusababisha hukumu zenye madhara kwa watu wasio
na hatia. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kuzishika amri ulizotufundisha,
ikiwa ni pamoja na kufuata roho ya sheria kadiri ya
mazingira. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wenye matatizo mbalimbali;
uyasikilize maombi yao, hasa ya wale walio katika
hatari ya kufa. Ee Bwana.
5. Ewe uliyetuahidia raha nafsini mwetu, uwapokee
marehemu wetu huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Yesu uliyesema nira yako ni laini na mzigo wako ni
mwepesi, uyapokee maombi yetu. Unayeishi na kutawala,
daima na milele. Amina.