IJUMAA JUMA 13 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.23:1-4,19;24:1-8,62-67
Umri wake Sara ulikuwa miaka mia na ishirini na saba, ndio umri wake Sara. Sara akafa katika
Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia Sara na kumwombolezea.
Akaondoka Ibrahimu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na bani Hethi, akinena, Mimi ni mgeni,
ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele
yangu. Basi baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe katika pango ya shamba la Makpela kuelekea
Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na Bwana
alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote. Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba
yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha
kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za
Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu
Isaka mke. Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii,
Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa
katika nyumba ya babaangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa
uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, anwe utamtwalia mwanangu mke tokea
huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini
usimrudishe mwanangu huko. Basi isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana laikaa
katika nchi ya kusini. Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake,
akaona, kuna ngamia wanakuja. Rebeka akainua macho, anaye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia.
Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana
wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda.
Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda;
Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamaake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.106:1-5 (K)1
1. Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
kwa maana fadhili zake ni za milele.
Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya Bwana,
kuzihubiri sifa zake zote.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.
2. Heri washikao hukumu,
Na kutenda haki sikuzote.
Ee Bwana, unikumbuke mimi,
Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako. (K)
3. Unijilie kwa wokovu wako,
Ili niuone wema wa wateule wako.
Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako,
Na kujisifu pamoja na watu wako. (K)
SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya!
Roho yangu inamngoja Bwana,
na Neno lake nimelitumainia.
Aleluya!
INJILI: Mt.9:9-13
Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia,
Nifuate. Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi
na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia
wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia,
aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake
maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, Yesu Kristo hakuja kuwaita wenye haki,
bali wenye dhambi. Kwa vile kuitikia wito wake ni kukubali
majukumu yanayoambatana na wito huo, tuombe
neema yake:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Kwa utii wa Mwanao aliouonesha mpaka msalabani,
uwajalie viongozi wote wa Kanisa neema ya utii wa
daima na udumifu katika kushika viapo vyao,
walivyovifanya mbele yako na mbele ya Kanisa
zima. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka watimize wajibu wao, hasa
katika kusimamia haki na maadili mema kwa raia
wao. Ee Bwana.
3. Wote wasiokukiri Wewe wajaliwe kutambua kuwa
wanafanana na wagonjwa wasiojijua na waongoke
na kupata tiba ya kiroho. Ee Bwana.
4. Utuwezeshe kuwahurumia na kuwarekebisha
wakosefu; kama alivyofanya Mwanao, Yesu
Kristo, apendaye rehema na siyo sadaka. Ee Bwana.
5. Uwaite marehemu wetu wapate kushiriki karamu yako
isiyo na mwisho huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu mpaji wa vyote, uyapokee maombi yetu. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.