IJUMAA JUMA 10 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 2Kor.4:7–15
Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka
kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali
hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; sikuzote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu,
ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai, sikuzote twatolewa
tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti.
Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu. Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile
ya Imani; kama ilivyoandikwa, Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na kwa
sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na
Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo
ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.116:10–11,15–19 (K)7
1. Naliamini, kwa maana nitasema,
Mimi naliteswa sana.
Mimi nalisema kwa haraka yangu,
Wanadamu wote ni waongo.
(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, Ee Bwana.
2. Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako,
Umevifungua vifungo vyangu. (K)
3. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana;
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote. (K)
SHANGILIO: 2Tim.1:10
Aleluya, aleluya!
Mwokozi wetu Yesu Kristu alibatili mauti,
na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya!
INJILI: Mt.5:27-32
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia,
Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako
la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja
kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha,
ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee, wala mwili wako mzima
usitupwe katika jehanum. Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; lakini
mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa
mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa maisha, mateso, kifo, ufufuko na kupaa
kwake mbinguni, Yesu ametuonesha njia nzima ya
wokovu wetu. Tuombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wa Kanisa wasikatishwe tamaa na dhiki au
dhoruba zinazolisonga Kanisa, bali wawe tayari kufa
kwa ajili ya kumfuasa Kristo Yesu. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka ya kiserikali wathamini
uhuru wa dini na mamlaka ya manabii wako kwa
watu wote, wakubwa kwa wadogo. Ee Bwana.
3. Mifumo ya maisha yasiyo ya kidini isiwe kikwazo
kwa imani yetu, bali ilingane na sheria yako ya milele.
Ee Bwana.
4. Sisi sote tulio hai tujaliwe kutolea daima maisha na
nafsi zetu kwa ajili ya Yesu, ili uzima wake udhihirishwe
katika miili yetu ipatikanayo na mauti. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapokelewe mbinguni na Mwanao
aliyekufa, ili watu wote wapate kuokoka. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetualika kuzing'oa pingamizi zote zinazoweza
kututia dhambini, uyapokee maombi yetu. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.