Generic placeholder image

DES. 17 JUMATANO JUMA LA 3 MAJILIO
MASIFU YA ASUBUHI

ANTIFONA YA MWALIKO:
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

Ant. ya Mwaliko
Bwana yu karibu: njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI tazama pia AU
3
Mwana milele pamoja na Baba,
Muoneni mzao wa bikira;
Kristo alijifanya mtumishi
Ili awakomboe watu wake.

Uinuke, Ewe Binti Sion
Mfalme mchanga msalimu;
Mioyo yenu iliyo migumu
Isidharau huruma ya Yesu.

Matendo ya giza na yatoroke
Kabla asubuhi haijaja,
Maana lazima dhambi tuache
Tu'tumikie Mwana wa Bikira.

Tumwimbie kwa shangwe na furaha
Kristo aliyetufanya huru;
Kadhalika tumtukuze Baba,
Pia naye Roho Mtakatifu.
Charles Coffin 1676-1749

AU
4
Haya Emanueli ufike
Tuokoa sisi utumwani,
Pweke tunalia ugenini
Hadi Mungu Mwana atokee.
Furahi ewe Israeli,
Atakujia Emanueli.

Njoo sasa Hekima wa juu,
Upangaye yote kwa ukuu;
Tuoneshe ya elimu njia,
Utufunze kuifuatia.
Furahi ewe Israeli,
Atakujia Emanueli.

Ufike sasa Bwana Mwenyezi,
Mlimani Sinai zamani
Kwa vitisho na enzi winguni,
Ulilipa taifa sheria.
Furahi ewe Israeli,
Atakujia Emanueli.

AU
5
Njoo Fimbo ya Shina la Yese,
Waokoe na kila adui
Watumainio wokovu wako,
Jalia wayashinde mauti.
Furahi ewe Israeli,
Atakujia Emanueli.

Ewe Ufunguo wa Daudi,
Tufungulie lango la mbingu;
Linda njia iendayo huko,
Sisi tupite bila taabu.
Furahi ewe Israeli,
Atakujia Emanueli.

Shuka sasa chanzo cha mchana,
Karibia utuchangamshe;
Tawanya mashaka ya usiku,
Kiza cha kifo kitokomee.
Furahi ewe Israeli,
Atakujia Emanueli.

Mtamaniwa na mataifa,
Unganisha mioyo ya watu;
Mgawanyiko sasa uishe,
Uwe Mfalme wa Amani.
Furahi ewe Israeli,
Atakujia Emanueli.

ANT. I: Bwana aliye na uwezo wote, atakuja kutoka Sion, kuwaokoa watu wake.

Zab.86 Kuomba msaada
Atukuzwe Mungu... mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote (2Kor.1:3-4)

Unisikilize, Ee Mungu, unitegee sikio,*
maana mimi ni fukara na mnyonge.

Uilinde roho yangu, maana mimi ni mchaji wako;*
uniokoe mimi mtumishi wako, ninayekutegemea.

Wewe ni Mungu wangu; basi, unionee huruma.*
Mimi ninakulilia mchana kutwa.

Unifurahishe mimi mtumishi wako, Ee Mungu,*
maana sala zangu nazielekeza kwako.

Wewe, Ee Bwana, u mwema na mwenye huruma;*
umejaa upendo mkuu kwa wote wanaokuomba.

Usikie, Ee Mungu, sala yangu;*
uangalie kilio cha ombi langu.

Siku za taabu nakuita,*
maana wewe wanisikiliza.

Ee Bwana, hakuna Mungu aliye kama wewe;*
hakuna awezaye kufanya unayofanya wewe.

Mataifa yote uliyoyaumba yatakuja na kukuabudu;*
yatatangaza ukuu wa jina lako.

Wewe ni mwenye enzi kuu, wafanya miujiza;*
wewe ndiwe Mungu peke yako.

Unifundishe, Ee Mungu, mwongozo wako,/
nami nitaufuata kwa uaminifu;*
uongoze moyo wangu nikuheshimu.

Nitakusifu, Ee Bwana, Mungu wangu, kwa moyo wote;*
nitatangaza ukuu wa jina lako hata milele.

Upendo wako ni mkuu mno!*
Umeniokoa kutoka chini kuzimu.

Ee Mungu, wenye kiburi wamenikabili;/
kundi la watu wakatili wanataka kuniua,*
watu ambao hawakujali wewe hata kidogo.

Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa huruma na mapendo;*
wewe ni mvumilivu, mpole na mwaminifu.

Unigeukie, unihurumie;/
unijalie nguvu yako, unisalimishe,*
mimi niliye mtumishi wako kama mama yangu.

Unioneshe ishara ya wema wako, Ee Mungu,/
ili wale wanaonichukia waaibike,*
wakiona wewe umenisaidia na kunifariji.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Bwana aliye na uwezo wote, atakuja kutoka Sion, kuwaokoa watu wake.

ANT. II: Sitaacha kusema juu ya Sion, mpaka hapo Mtakatifu wake atakapong'aa kama nuru.

WIMBO: Isa.33:13-16 Mungu atatawala kwa haki
Ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali, na kwa ajili ya wowote wale ambao Bwana Mungu wetu atawaita kwake. (Mate.2:39)

Sikieni ninyi mlio mbali, niliyoyatenda;/.
na ninyi mlio karibu,*
kirini uweza wangu.

Wenye dhambi walio katika Sion wanaogopa;*
tetemeko limewashika wasiomcha Mungu;

Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao;*
ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?

Ni yeye aendaye kwa haki,*
anenaye maneno ya adili;

ni yeye anayedharau faida*
ipatikanayo kwa dhuluma;

akung'utaye mikono yake*
asipokee rushwa;

azibaye masikio yake*
asisikie habari za damu;

afumbaye macho yake*
asitazame uovu.

Huyu ndiye atakayekaa juu;*
majabali ni ngome yake;

atapewa chakula chake;*
maji yake hayatakoma.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Sitaacha kusema juu ya Sion, mpaka hapo Mtakatifu wake atakapong'aa kama nuru.

ANT. III: Roho wa Bwana yu juu yangu, amenituma kuwatangazia maskini Habari Njema.

Zab.98 Mungu mtawala dunia yote
Zaburi hii yaeleza ujio wa kwanza wa Bwana, na imani ya mataifa yote (Mt. Athanasius)

Mwimbieni Mungu, wimbo mpya,*
kwa maana ametenda mambo ya ajabu!

Kwa nguvu na enzi yake takatifu*
amejipatia ushindi.

Mungu ameonesha ushindi wake;*
ameyadhihirishia mataifa uwezo wake wa kuokoa.

Ameshika ahadi aliyowapa watu wa Israeli,*
kwa upendo mkuu na uaminifu kwao.

Pande zote za dunia*
zimeuona ushindi wa Mungu wetu.

Dunia yote imshangilie Mungu;*
imsifu kwa nyimbo na vigelegele.

Msifuni Mungu kwa shangwe,*
kwa sauti za kinubi na zeze.

Mpigieni vigelegele Mungu mfalme wetu,*
mshangilieni kwa tarumbeta na sauti ya baragumu.

Bahari ivume na vyote vilivyomo;*
dunia na wote waishio ndani yake.

Enyi mito, pigeni makofi;*
enyi vilima, imbeni pamoja kwa shangwe.

Shangilieni mbele ya Mungu,*
maana anakuja kutawala dunia.

Atauhukumu ulimwengu kwa haki,*
na watu atawatawala kwa uadilifu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Roho wa Bwana yu juu yangu, amenituma kuwatangazia maskini Habari Njema.

SOMO: Isa.11:1-2
Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya BWANA atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA.

KIITIKIZANO
K. Utukufu wa Bwana utakung'aria, Ee Yerusalemu. Kama jua Bwana atachomoza juu yako. (W. Warudie)
K. Utukufu wake utajitokeza katikati yako.
W. Kama jua Bwana atachomoza juu yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utukufu...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Jueni kwamba utawala wa Mungu u karibu; hakika Bwana hatakawia.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake

Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Jueni kwamba utawala wa Mungu u karibu; hakika Bwana hatakawia.

MAOMBI
Bwana, Mungu wetu, yu aja: tuondoe hofu, na kwa matumaini tungojee mambo ya mbele.
W. Utawala wako ufike.

Bwana, umeumba vitu vyote, na unavifanya upya:
- ulimwengu wote wadhihirisha kazi yako. (W.)

Umetujalia uwezo wa kuvitiisha viumbe vyote;
- utuwezeshe, kwa njia ya kazi zetu, kushiriki kazi yako ya kuumba. (W.)

Tunaomba wafarijike na kueleweka vizuri,
- wale wote wanaowahudumia wagonjwa na watu wanaoteseka. (W.)

Utubariki tunapofanya kazi;
- utujalie imani mpaka mwisho, hapo kazi zetu zitakapotunukiwa zawadi. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Baba, kwa mapenzi yako Mwanao alitwaa ubinadamu wetu ambao wewe uliuumba na kuukomboa. Tunaomba, Neno wako aliyejipatia mwili kwa njia ya Bikira Maria na kuwa mwandamu kama sisi, atushirikishe umungu wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.