Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 6 PASAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya

Zab.119:65-72 IX Umuhimu wa sheria ya Mungu
Umenitendea vema mimi mtumishi wako,*
kama ulivyoahidi, Ee Mungu.

Unipe hekima na maarifa,*
maana nina imani na amri zako.

Kabla ya kuniadhibu nilikosa,*
lakini sasa nashika agizo lako.

Wewe ni mwema na mfadhili;*
unifundishe kanuni zako.

Wenye kiburi wanasema uwongo juu yangu,*
lakini nashika amri zako kwa moyo wote.

Watu hao hawana akili,*
lakini mimi nafurahia sheria yako.

Nimefaidika kutokana na taabu yangu,*
maana imenifanya nijifunze amri zako.

Sheria uliyoweka ni muhimu zaidi kwangu*
kuliko mali zote za dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.56:1-6,8-13 Kumtumainia Mungu
Kristo ameoneshwa akiteseka (Mt. Jeromu)

Ee Mungu, unionee huruma,/
maana watu wananivamia.*
Wakati wote adui zangu wanizingira.

Mchana kutwa adui zangu wanishambulia;*
ni wengi mno hao wanaonipiga vita.

Ee Mungu, hofu inaponishika,*
mimi nakutumainia wewe.

Namtumainia Mungu, wala siogopi./
Ninamsifu kwa ajili ya ahadi yake.*
Binadamu watanifanya nini?

Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu;*
mawazo yao yote ni ya kunidhuru.

Wanakutana kupanga na kunivizia;/
wanachunguza yote nifanyayo;*
wananiotea kwa shabaha ya kuniua.

Ee Mungu, uwalipe kwa kadiri ya uovu wao,*
uwaangushe hao waovu kwa hasira yako.

Wewe wakujua kutangatanga kwangu;/.
umeweka kumbukumbu ya machozi yangu.*
Je, yote si yamo kitabuni mwako?

Kila mara ninapokuomba msaada wako,/
adui zangu wanarudishwa nyuma.*
Najua kwa hakika: Mungu yuko upande wangu.

Sheria uliyoweka ni muhimu zaidi kwangu*
kuliko mali zote za dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.57 Kuomba msaada
Zaburi hii yaeleza mateso ya Bwana (Mt. Augustino)

Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,*
kwako ninakimbilia usalama.

Kivulini mwa mabawa yako, napata usalama,*
hata hapo dhoruba kali itakapopita.

Namlilia Mungu Mkuu,*
Mungu anijaliaye kila kitu.

Atanisikiliza kutoka mbinguni na kuniokoa;/
atawashinda hao wenye kunidhulumu.*
Mungu atanionesha mapendo na uaminifu wake.

Adui wanizunguka kama simba wala watu;/
meno yao ni kama mikuki na mishale,*
ndimi zao ni kama panga kali.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu,*
utukufu wako uenee duniani kote.

Adui wamenitegea wavu waninase,*
nami nasononeka kwa huzuni.

wamenichimbia shimo njiani,*
lakini wao wenyewe wametumbukia humo.

Niko imara, Ee Mungu, niko imara;*
nitaimba na kukushangilia!

Amka, ee nafsi yangu!/
Amkeni, enyi zeze na kinubi!*
Nitayaamsha mapambazuko!

Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa;*
nitakuimbia sifa kati ya watu.

Upendo wako mkuu waenea hata mbinguni,*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu;/
utukufu wako uenee duniani kote.*
Kinanda na kinubi, amkeni, nitaiamsha alfajiri.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Kor.12:13
Sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja.

K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Tito3:5b-7
Mungu alitukomboa kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mkombozi wetu, ili kwa neema yake tupate uhusiano mwema na Mungu, na kuupokea uzima wa milele tunaoutumainia.

K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Kol.1:12-14
Na, kwa furaha mshukuruni Baba aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale Mungu aliyowawekea watu wake katika Utawala wa mwanga. Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika Utawala wa Mwanae mpenzi, ambaye kwa njia yake tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.

K. Kaa nasi, Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.

SALA:
Tuombe: Mungu Baba yetu, umewapa watu wako mwokozi: uijaze mioyo yetu shukrani na sifa daima, kwa vile Kristo Bwana amefufuka kutoka wafu. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.