ALHAMISI JUMA LA 6 PASAKA
MASOMO

SOMO: Mdo.18:1-8
Siku zile, Paulo alitoka Athene akafika Korintho. Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzaliwa wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema. Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani. Hata Sila na Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo. Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung’uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-4(K)2
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.

(K) Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa:
Au:
Aleluya.

2. Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

SHANGILIO: Lk.24:25-26
Aleluya, aleluya,
Ilimpasa Kristo kupata mateso haya
na kuingia katika utukufu wake.
Aleluya.

INJILI: Yn.16:16-20
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona. Basi baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba? Basi walisema, neno gani hilo asemalo; hilo, Bado kitambo kidogo? Hatujui asemalo. Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.

MAOMBI
Ndugu, kumcha Mungu ni paji muhimu kwa kila mwanadamu. Mara nyingi tunashindwa kulitekeleza hilo kwa sababu ya kusongwa na mambo mengine ya maisha. Tuombe neema yake Mungu:

Kiitikio: Utujalie neema yako.
1. Uwajalie viongozi wetu wa Kanisa amani na furaha katika kulihubiri neno lako. Ee Bwana.

2. Kwa mwanga wa Pasaka, uziangaze dhamiri za wote wasiokukiri wewe Mungu, ili walisikie neno lako, waamini na kubatizwa. Ee Bwana.

3. Wote wenye matatizo ya kimwili na kiroho waonje uwepo wa Mwanao mwenye kugeuza huzuni zetu kuwa furaha. Ee Bwana.

4. Sauti ya Mwanao isemayo “Bado kitambo kidogo nanyi mtaniona“ na isikike leo kwa ndugu zetu marehemu. Ee Bwana.

Tunaomba hayo yote kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.