ALHAMISI JUMA LA 6 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana amefufuka kweli, aleluya.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!
Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!
Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!
Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534
2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ
3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.
Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876
4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.
Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.
Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.
Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.
Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.
Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.
Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.
Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7
5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.
Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.
Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal
6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.
Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.
Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750
7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.
Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.
Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.
Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.
Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695
ANT. I: Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, aleluya.
Zab.80 Kwa ajili ya urekebisho wa Israeli
Njoo, Bwana Yesu (Ufu.22:20)
Utusikilize, ewe Mchungaji wa Israeli,*
unayewaongoza watu wako, Yosefu, kama kondoo.
Ewe ukaaye juu ya viumbe vyenye mabawa,/
ujioneshe kwa Efraimu, Benyamini na Manase.*
Uoneshe nguvu yako, uje ukatuokoe!
Uturekebishe, Ee Mungu;*
utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.
Ee Mungu, Mungu mwenye nguvu,*
hata lini utazikasirikia sala za watu wako?
Umefanya huzuni iwe chakula chetu;*
umetunywesha machozi kwa wingi.
Umetufanya kisa cha ubishi kwa jirani zetu;*
adui zetu wanatudhihaki.
Ee Mungu mwenye nguvu, uturekebishe,*
utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.
Ulileta mzabibu mmoja kutoka Misri;/
ukawafukuza watu wa mataifa mengine,*
na kuupanda katika nchi yao.
Uliupalilia upate kukua,*
nao ukatoa mizizi, ukaenea kote nchini.
Uliifunika milima kwa kivuli chake,*
na matawi yake yakawa kama mierezi mikubwa.
Matawi yake yalienea mpaka baharini;*
machipukizi yake mpaka kando ya mto Eufrate.
Mbona ulibomoa kuta zilizouzunguka?*
Sasa kila apitaye anachuma zabibu zake;
nguruwe-mwitu wanauharibu,*
na wanyama wa porini wanautafuna!
Ee Mungu mwenye nguvu, utugeukie tena!*
Uangalie toka mbinguni, uutunze mzabibu huo.
Uulinde huo mche ulioupanda kwa mkono wako;*
hicho kichipukizi ulichokisitawisha.
Watu walioukata na kuuteketeza,*
uwatazame kwa ukali, waangamie.
Mkono wako umkinge huyo uliyemfadhili;*
huyo uliyemteua kwa ajili yako.
Hatutakuacha na kukuasi tena;*
utujalie uzima, nasi tutakusifu.
Ee Mungu, Mungu mwenye nguvu, uturekebishe;*
utuangalie kwa wema, nasi tutasalimika.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, aleluya.
ANT. II: Kwa furaha mteteka maji katika visima vya Mwokozi, aleluya.
WIMBO: Isa.12:1-6 Furaha ya watu waliokombolewa
Aliye na kiu na aje kwangu anywe (Yoh.7:37)
Ee BWANA, nitakushukuru wewe;*
Kwa kuwa ijapokuwa ulinikasirikia,
Hasira yako imegeukia mbali,*
Nawe unanifariji moyo.
Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;*
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana BWANA ni nguvu zangu na wimbo wangu;*
Naye amekuwa wokovu wangu.
Basi, kwa furaha mtateka maji*
Katika visima vya wokovu.
Na katika siku hiyo mtasema,*
Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,*
Litajeni jina lake kuwa limetukuka.
Mwimbieni BWANA; kwa kuwa ametenda makuu;*
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sion;*
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Kwa furaha mteteka maji katika visima vya Mwokozi, aleluya.
ANT. III: Bwana ametulisha ngano bora, akatushibisha asali itokayo mwambani.
Zab.81 Wimbo wa sikukuu
Basi, ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo
na asiyeamini (Ebr.3:12)
Mshangilieni Mungu, mlinzi wetu,*
mwimbieni sifa Mungu wa Yakobo;
Vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma,*
chezeni kinubi na zeze zenye sauti nzuri.
Pigeni baragumu la mwezi mpya,*
na la mwezi mpevu, sikukuu yetu.
Hiyo ndiyo kanuni katika Israeli;*
hilo ndilo agizo la Mungu wa Yakobo.
Alimpa Yosefu agizo hilo,*
alipoishambulia nchi ya Misri.
Nasikia sauti nisiyoitambua ikisema:/
"Mimi nimekutua mizigo yako mabegani,*
nimekuondolea matofali uliyochukua mikononi.
Ukiwa shidani uliniita, nami nikakuokoa./
Nikiwa nimejificha katika ngurumo nilikujibu.*
Nilikujaribu kwenye maji ya Meriba.
Enyi watu wangu, sikilizeni onyo langu.*
Laiti ungenisikiliza, ee Israeli!
Asiwepo kwako mungu wa kigeni;*
usiabudu kamwe mungu mwingine.
Mimi ndimi Mungu, Mungu wako,/
niliyekuhamisha kutoka nchi ya Misri.*
Fungua kinywa chako, nami nitakulisha.
Lakini watu wangu hawakunisikiliza;*
Israeli hakupenda kunitii mimi.
Basi, nikawaacha wabaki na ukaidi wao;*
wafuate mashauri yao wenyewe.
Laiti watu wangu wangenisikiliza!*
Laiti Israeli angefuata mwongozo wangu!
Mara ningewaangamiza adui zao;*
ningewashinda wadhalimu wao.
Wanichukiao wangenipigia magoti kwa hofu,*
na adhabu yao ingekuwa ya milele.
Lakini wewe ningekulisha kwa ngano bora,*
na kukushibisha kwa asali ya mwambani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Bwana ametulisha ngano bora, akatushibisha asali itokayo
mwambani.
SOMO: Rom.8:10-11
Kama Kristo yuko ndani yenu, ingawa miili yenu itakufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye
uhai, kwa sababu mmefanywa kuwa wenye uhusiano mwema na Mungu. Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua
Yesu katika wafu anaishi ndani yenu, basi, huyo aliyemfufua Kristo katika wafu ataipa uzima
miili yenu yenye hali ya kufa, atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.
KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona, asema Bwana; na baada ya kitambo kidogo mtaniona tena,
kwa kuwa nakwenda kwa Baba, aleluya.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona, asema Bwana; na baada
ya kitambo kidogo mtaniona tena, kwa kuwa nakwenda kwa Baba, aleluya.
MAOMBI
Kwa imani na matumaini, tumwombe Mungu Baba yetu. Katika Kristo amewapa watoto wake wote amana
ya ufufuko.
W. Bwana Yesu na awe uzima wetu.
Baba, kwa mnara wa moto uliwaongoza watu wako jangwani;
- Kristo mfufuka na awe nuru ya maisha yetu. (W.)
Kwa sauti ya Musa ulizungumza mlimani;
- Kristo mfufuka na awe neno letu la uzima. (W.)
Kwa zawadi ya manna uliwalisha watu wako waliokuwa safarini;
- Kristo mfufuka na awe mkate wetu utokao mbinguni. (W.)
Uliufanya mwamba utoe maji ili uwaokoe watoto wako;
- Kristo mfufuka na atujaze Roho wake. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi
wetu: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Baba yetu, umewapa watu wako mwokozi: uijaze mioyo yetu shukrani na sifa daima, kwa
vile Kristo Bwana amefufuka kutoka wafu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,
Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.