ALHAMISI JUMA LA 5 PASAKA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
Zab.119:17-24 III Furaha katika sheria ya Mungu
Unifadhili mimi mtumishi wako,*
nipate kuishi na kushika agizo lako.
Uyafumbue macho yangu,*
niyaone maajabu ya sheria yako.
Mimi ni mkimbizi tu hapa duniani;*
usinifiche maagizo yako.
Roho yangu yaugua kwa hamu kubwa*
ya kutaka kujua daima hukumu zako.
Wewe wawakemea watu wenye kiburi;*
walaaniwe wanaokiuka amri zako.
Uniepushe na matusi na madharau yao,*
maana nimezishika kanuni zako.
Hata kama wakuu wanakula njama dhidi yangu,*
mimi mtumishi wako nitajifunza maagizo yako.
Amri zako ni furaha yangu;*
hunipa ushauri mwema.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.25 Kuomba uongozi na ulinzi
Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa (Rom.5:5)
I
Kwako naja, Ee Mungu, kwa moyo wangu wote!*
Nakutumainia wewe, Ee Mungu wangu,
usiniache niaibike;*
adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu.
Wote wale wakutegemeao hawataaibika;*
lakini wanaokuasi ovyo wataaibika.
Ee Mungu, unijulishe njia yako;*
naam, unipe mwongozo wako.
Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha,/
kwani wewe ni Mungu unayeniokoa;*
ninakutumainia wewe daima.
Ee Mungu, uukumbuke wema wako mkuu;/
uukumbuke na upendo wako mkuu,*
maana vimekuwako tangu milele.
Unisamehe dhambi na makosa ya ujana wangu;/
unikumbuke kadiri ya upendo wako mkuu,*
kwa ajili ya wema wako, Ee Mwenyezi.
Mungu ni mwema na mwadilifu;*
huwapa wakosefu mwongozo.
Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu;*
naam, huwafundisha hao njia yake.
Mungu huwalinda kwa upendo mkuu na uaminifu,*
wale wanaozingatia matakwa ya agano lake.
Kwa heshima ya jina lako, Ee Mungu,*
unisamehe uovu wangu, kwani ni mkubwa.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Kila mtu anayemcha Mungu,*
atafunzwa naye mwongozo wa kufuata.
Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima;*
na watoto wake watamiliki nchi.
Mungu ni msiri wa watu wanaomcha;*
yeye huwajulisha hao agano lake.
Namtazamia Mungu daima anisaidie;*
yeye peke yake ataniokoa mtegoni.
Uniangalie, Ee Mungu, unionee huruma,*
kwa sababu mimi niko peke yangu, na mnyonge.
Uniondolee mahangaiko yangu;*
uniokoe katika taabu zangu.
Uangalie unyonge wangu na dhiki yangu;*
unisamehe dhambi zangu zote.
Angalia jinsi walivyo wengi adui zangu;*
ona jinsi wanavyonichukia mno.
Uyalinde maisha yangu na kuniokoa;*
nakukimbilia wewe, usikubali niaibike.
Wema na uadilifu vinihifadhi,*
maana ninakutumainia wewe.
Ee Mungu, uwaokoe watu wako, Israeli;*
uwaokoe katika taabu zao zote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: 1Kor.12:13
Sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa
Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja.
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Tito3:5b-7
Mungu alitukomboa kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe
upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo
kwa njia ya Yesu Kristo, Mkombozi wetu, ili kwa neema yake tupate uhusiano mwema na Mungu, na
kuupokea uzima wa milele tunaoutumainia.
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Kol.1:12-14
Na, kwa furaha mshukuruni Baba aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale
Mungu aliyowawekea watu wake katika Utawala wa mwanga. Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya
giza, akatuleta salama katika Utawala wa Mwanae mpenzi, ambaye kwa njia yake tunakombolewa,
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
K. Kaa nasi, Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.
SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, tulikuwa wenye dhambi, na neema yako ikatufanya tuwe watakatifu; tulikuwa
bila matumaini, nawe ukatujaza furaha. Utusaidie kwa kazi yako ya kuokoa, na ukae nasi katika
neema zako. Utuwezeshe kudumu katika utakatifu utokanao na imani. Tunaomba hayo kwa njia ya
Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.