Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 5 PASAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!

Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!

Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!

Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534

2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ

3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.

Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876

4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.

Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.

Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.

Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.

Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.

Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.

Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.

Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7

5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.

Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.

Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal

6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.

Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.

Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750

7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.

Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.

Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.

Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.

Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695

ANT. I: Uligeza huzuni yangu kuwa furaha, aleluya.

Zab.30 Sala ya Shukrani
Kristo, baada ya ufufuko wake mtukufu, amshukuru Baba yake (Kasiani)

Nakusifu, Ee Mungu, maana umeniokoa,*
wala hukuwaacha adui zangu wanisimange.

Ee Mungu, Mungu wangu,*
nilikulilia, nawe ukaniponya.

Ee Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu;*
umenitoa katika msafara wa waendao Shimoni.

Mwimbieni Mungu sifa, enyi watakatifu wake;*
kumbukeni utakatifu wake na kumsifu.

Hasira yake hudumu kitambo kidogo,*
lakini fadhili yake hudumu milele.

Kilio huwapo jioni,*
lakini asubuhi husikika sauti ya furaha.

Mimi katika usitawi wangu, nilisema:*
"Kamwe sitatikisika!"

Ee Mungu, kwa fadhili yako,*
umeniimarisha kama mlima mkubwa.

Lakini ukajificha mbali nami,*
nami nikaogopa.

Nilikulilia wewe, Ee Mungu;*
nilikusihi wewe Mungu:

“Je, nikifa utapata faida gani?*
Kuna faida gani nikishuka Shimoni?

Je, waliokufa wanaweza kukusifu?*
Je, wanaweza kutangaza wema wako mkuu?

Usikie, Ee Mungu, unihurumie,*
Ee Mungu, unisaidie!"

Wewe umegeuza ombolezo langu*
kuwa ngoma ya furaha;

umeniondolea huzuni yangu,*
ukanijalia furaha tele tele.

Basi, sitakaa kimya,*
bali nitakuimbia sifa.

Ee Mungu, Mungu wangu,*
nitakushukuru milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: EUligeza huzuni yangu kuwa furaha, aleluya.

ANT. II: Tumepatanishwa na Mungu kwa kifo cha Mwanae, aleluya.

Zab.32 Maondoleo ya dhambi
Daudi asema, ana heri yule ambaye Mungu amemfanya awe na uhusiano mwema naye bila kujali matendo yake (Rom.4:6)

Heri yao waliosamehewa dhambi zao,*
ambao makosa yao yameondolewa.

Heri yake mtu aliyesamehewa kosa na Mungu,*
mtu ambaye hana hila moyoni mwake.

Wakati nilipokuwa sijakiri makosa yangu,*
nilikuwa nimedhoofika kwa kulia mchana kutwa.

Mchana na usiku uliniadhibu, Ee Mungu;/
nikafyonzwa nguvu zangu,*
kama maji wakati wa kiangazi.

Kisha nikaziungama dhambi zangu kwako;*
wala sikuuficha uovu wangu.

Niliazimu kukiri makosa yangu kwako, Ee Mungu;*
ndipo nawe ukanisamehe dhambi zangu.

Kwa hiyo, kila mcha Mungu, akuombe wakati wa shida;*
yakitokea mafuriko ya taabu hayatamfikia.

Wewe ndiwe kimbilio langu;/
wewe wanilinda katika taabu.*
Nimejawa shangwe maana umenikomboa.

Mungu asema, "Nitakuonesha njia ya kufuata.*
Nitakufundisha na kukuelekeza.

Usiwe mpumbavu kama farasi au nyumbu,*
wasiotawalika ila kwa lijamu na hatamu."

Watu waovu watapata mateso mengi;/
lakini wanaomtumaini Mungu*
wanalindwa kwa upendo wake mkuu.

Enyi waadilifu, furahieni na kushangilia/
aliyotenda Mungu;*
enyi mlio wanyofu, pigeni vigelegele vya furaha.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Tumepatanishwa na Mungu kwa kifo cha Mwanae, aleluya.

ANT. III: Bwana, ni nani aliye sawa nawe katika utukufu, nguvu na utakatifu? Aleluya.

WIMBO: Ufu.11:17-18;12:10b-1
Bwana Mungu Mwenyezi,*
uliyeko na uliyekuwako!

Tunakushukuru,/
maana umetumia nguvu yako kuu*
ukaanza kutawala!

Watu wa mataifa waliwaka hasira,/
maana wakati wa ghadhabu yako umefika,*
wakati wa kuwahukumu wafu.

Ndio wakati wa kuwatuza*
watumishi wako manabii,

watu wako na wote wanaolitukuza jina lako,*
wakubwa kwa wadogo.

Sasa wokovu utokao kwa Mungu umefika!/
Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika.*
Na Masiha wake ameonesha mamlaka yake!

Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu,*
aliyesimama mbele ya Mungu

akiwashtaki usiku na mchana,*
sasa ametupwa nje.

Ndugu zetu wameshinda/
kwa damu ya Mwanakondoo*
na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza;

maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana,*
wakawa tayari kufa.

Kwa sababu hiyo furahini enyi mbingu*
na vyote vilivyomo ndani yenu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Bwana, ni nani aliye sawa nawe katika utukufu, nguvu na utakatifu? Aleluya.

SOMO: 1Pet.3:18,22
Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke ninyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili, lakini akafanywa hai kiroho; ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.

KIITIKIZANO
K. Wanafunzi walifurahi,aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Walipomwona Bwana.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wanafunzi...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Nimewaambieni hayo ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu ikamilike, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Nimewaambieni hayo ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu ikamilike, aleluya.

MAOMBI
Kristo amefufuka kutoka wafu, wa kwanza kufufuka miongoni mwa wote waliokufa. Na tumtolee masifu yetu.
W. Bwana Mfufuka, utusikie.

Bwana, ulikumbuke Kanisa, ulilojenga juu ya msingi wa mitume;
- uwabariki wote wanaokusadiki wewe. (W.)

Wewe ndiwe mganga wa mwili na roho;
- utuletee wokovu wako. (W.)

Uwafariji wagonjwa na kuwapa nguvu mpya;
- uwaondolee maumivu na mahangaiko yote. (W.)

Uwasaidie wenye uchungu na wanaokandamizwa;
- kwa mapendo yako uwategemeze maskini. (W.)

Kwa msalaba na ufufuko wako umejipatia uzima wa milele;
- uwajalie marehemu wetu furaha za utawala wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tumwombe Baba, kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, tulikuwa wenye dhambi, na neema yako ikatufanya tuwe watakatifu; tulikuwa bila matumaini, nawe ukatujaza furaha. Utusaidie kwa kazi yako ya kuokoa, na ukae nasi katika neema zako. Utuwezeshe kudumu katika utakatifu utokanao na imani. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.