Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 5 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana amefufuka kweli, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!

Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!

Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!

Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534

2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ

3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.

Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876

4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.

Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.

Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.

Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.

Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.

Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.

Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.

Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7

5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.

Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.

Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal

6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.

Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.

Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750

7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.

Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.

Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.

Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.

Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695

ANT. I: Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, aleluya.

Zab.57 Kuomba msaada
Zaburi hii hutukuza mateso ya Kristo (Mt. Augustino)

Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,*
kwako ninakimbilia usalama.

Kivulini mwa mabawa yako, napata usalama,*
hata hapo dhoruba kali itakapopita.

Namlilia Mungu Mkuu,*
Mungu anijaliaye kila kitu.

Atanisikiliza kutoka mbinguni na kuniokoa;/
atawashinda hao wenye kunidhulumu.*
Mungu atanionesha mapendo na uaminifu wake.

Adui wanizunguka kama simba wala watu;/
meno yao ni kama mikuki na mishale,*
ndimi zao ni kama panga kali.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu,*
utukufu wako uenee duniani kote.

Adui wamenitegea wavu waninase,*
nami nasononeka kwa huzuni.

Wamenichimbia shimo njiani,*
lakini wao wenyewe wametumbukia humo.

Niko imara, Ee Mungu, niko imara;*
nitaimba na kukushangilia!

Amka, ee nafsi yangu!/
Amkeni, enyi zeze na kinubi!*
Nitayaamsha mapambazuko!

Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa;*
nitakuimbia sifa kati ya watu.

Upendo wako mkuu waenea hata mbinguni,*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu;*
utukufu wako uenee duniani kote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, aleluya.

ANT. II: Bwana amewakomboa watu wake, aleluya.

WIMBO: Yer.31:10-14 Furaha ya watu waliokombolewa
Yesu ilimpasa kufa kusudi awaunganishe watoto wa Mungu waliokuwa wametawanyika (Yoh.11:51-52)

Lisikieni neno la BWANA, enyi mataifa,*
litangazeni visiwani mbali; mkaseme,

Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda,*
kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Kwa maana BWANA amemweka huru Yakobo,*
amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.

Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sion,*
wataukimbilia wema wa BWANA,

nafaka, na divai na mafuta,*
na wachanga wa kondoo na wa ng'ombe;

na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji;*
wala hawatahuzunika tena kabisa.

Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,*
na vijana na wazee pamoja;

maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,/
nami nitawafariji, na kuwafurahisha*
waache huzuni zao.

Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono,*
na watu wangu watashiba kwa wema wangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana amewakomboa watu wake, aleluya.

ANT. III: Mungu yu pamoja nasi, Mungu wetu milele na milele, aleluya.

Zab.48 Sion mji wa Mungu
Akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionesha mji mtakatifu, yaani Yerusalemu (Ufu.21:10)

Mungu ni mkuu na wa kusifika sana,/
katika mji wa Mungu wetu,*
juu ya mlima wake mtakatifu.

Sion, mlima wa Mungu, ni mrefu na mzuri;*
mji wa mfalme mkuu ni furaha ya ulimwengu.

Katika ngome za mji Sion,*
Mungu amejionyesha kuwa mwamba wa usalama.

Wafalme walikusanyika,*
wakaanza kushambulia.

Lakini walipouona tu mji wa Sion, wakashangaa;*
akashikwa na hofu, wakatimua mbio.

Woga uliwashika wakaanza kuhangaika,*
wakawa kama mwanamke anayejifungua.

Uliwarusharusha kama meli katika dhoruba./
Yote tuliyosikia Mungu ametenda,*
sasa sisi wenyewe tumeyaona;

katika mji wa Mungu, Mungu mwenye nguvu,*
Mungu atauweka mji huo salama milele.

Ee Mungu, twautafakari upendo wako mkuu,*
tukiwa Hekaluni mwako.

Wewe wasifika kila mahali,/
sifa zako zaenea popote duniani.*
Wewe watawala kwa haki;

watu wa Sion wafurahi!/
Wewe watoa hukumu zilizo sawa;*
watu wa mji wa Yuda na washangilie!

Haya, nendeni Sion mkauzunguke,*
nendeni mkahesabu minara yake.

Zitazameni kuta zake na kuchunguza ngome zake;*
mpate kukisimulia kizazi kijacho, kwamba:

“Huyu ni Mungu, Mungu wetu milele!*
Atakuwa kiongozi wetu milele"!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mungu yu pamoja nasi, Mungu wetu milele na milele, aleluya.

SOMO: Rom.8:10-11
Kama Kristo yuko ndani yenu, ingawa miili yenu itakufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai, kwa sababu mmefanywa kuwa wenye uhusiano mwema na Mungu. Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu katika wafu anaishi ndani yenu, basi, huyo aliyemfufua Kristo katika wafu ataipa uzima miili yenu yenye hali ya kufa, atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.

KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Mkizishika amri zangu, mtabaki katika upendo wangu, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mkizishika amri zangu, mtabaki katika upendo wangu, aleluya.

MAOMBI
Tumtolee masifu yetu, Kristo aliyefufuka kutoka wafu, na ambaye anaishi daima katika Kanisa lake.
W. Bwana, kaa nasi daima.

Bwana, umeshinda dhambi na mauti;
- uwe kati yetu, pamoja na uzima wako wa milele. (W.)

Utujie na nguvu yako isiyolegea;
- na utudhihirishie maishani mwetu fadhili kuu za Mungu. (W.)

Wewe peke yako waweza kuwapatanisha watu, na kuwatia roho mpya;
- komesha magomvi yanayougawanya ulimwengu. (W.)

Ikuze imani yetu katika ushindi wako mkuu;
- utuwezeshe kupata nguvu kwa kutumaini kuona ujio wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, tulikuwa wenye dhambi, na neema yako ikatufanya tuwe watakatifu; tulikuwa bila matumaini, nawe ukatujaza furaha. Utusaidie kwa kazi yako ya kuokoa, na ukae nasi katika neema zako. Utuwezeshe kudumu katika utakatifu utokanao na imani. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.