ALHAMISI JUMA 5 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: Mwa.17:3-9
Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao. Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:4-9(K)8
1. Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake siku zote.
Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,
Miujiza yake na hukumu za kinywa chake.

(K) Analikumbuka agano lake milele.

2. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)

3. Analikumbuka agano lake milele;
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
Agano alilofanya na Ibrahimu,
Na uapo wake kwa Isaka. (K)

SHANGILIO: 2Kor.6:2
Tazama,
wakati uliokubalika ndio sasa,
tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.

INJILI: Yn.8:51-59
Yesu aliwaambia Wayahudi: Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele. Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng'amua ya kuwa una pepo. Ibrahimu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele. Wewe u mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani? Yesu akajibu, Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu. Wala ninyi hamkumjua; lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi; lakini namjua, na neno lake nalishika. Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi. Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu? Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko. Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.

MAOMBI
Ndugu, kutokana na uzao wa Ibrahimu tumempata Yesu Kristo Mkombozi wetu. Tunahitaji imani kama ya Ibrahimu, ili kupata wokovu. Basi, tuombe. Ee Mungu Baba yetu twakuomba:

Kiitikio: Mungu wa huruma utusikie.
1. Wazee wa Kanisa wazidi kuifundisha imani yetu ya kikristo, kuilinda na kuirithisha kwa vizazi vyote.

2. Wabatizwa wote wadumu katika imani tuliyoikiri siku ya Ubatizo ambapo tulikufa na kufufuka pamoja na Kristo.

3. Utujalie kulishika neno lako kiaminifu, ili tusione mauti milele.

4. Uwasamehe marehemu wetu makosa yao na kuwashirikisha uzima wa milele.

Ee Bwana Mungu, Mwanao alikujua wewe, ndiyo maana aliweza kukukiri mbele ya watu. Utuwezeshe nasi kulitukuza jina lako kwa unyenyekevu, ili watu wote wakujue, wakupende na wakaokoke milele. Amina.