ALHAMISI JUMA 34 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Dan.6:12-28
Mawaziri na maamiri walikusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.
Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia
sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote,
katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu,
akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika. Basi
wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa
Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila
siku. Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli;
akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme,
wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo
lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta
Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia
daima, yeye atakuponya. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia
muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika
habari za Danieli. Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda
havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa. Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa
haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa
sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai,
je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia
mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya
simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako,
Ee mfalme, sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu.
Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa
sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki
Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba
wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu. Ndipo
mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya
uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu. Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme
wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai,
adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho. Yeye
huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na
nguvu za simba.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.100 (K)Ufu.19:9
1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote,
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba.
(K) Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwanakondoo.
2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
3. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake. (K)
4. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)
SHANGILIO: 1Sam.3:9,Yn.6:68
Aleluya, aleluya!
Nena Bwana Wewe unayo maneno ya uzima wa milele
Aleluya!
INJILI: Lk.21:20-28
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo
jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia. Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na
walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie. Kwa kuwa siku hizo ndizo
za mapitilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa. Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika
siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida katika nchi, na hasira juu ya taifa hili. Wataanguka kwa
ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa
na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia. Tena, kutakuwa na ishara katika jua; na mwezi,
na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu
wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazama mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni
zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu
mwingi. Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi
wenu umekaribia.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu Wapendwa, Mungu huponya na kuokoa, na hutenda ishara na maajabu mbinguni na
duniani. Kwa hiyo, tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wa Kanisa wajaliwe hekima na busara ya pekee, wapate kuwaandaa vema
waamini wao kwa ujio wa Mwanao, na kuwaondolea hofu mioyoni mwao. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wasijiengue kwenye mwaliko wa karamu ya Mwana-Kondoo; na
wawaongoze watu wao kadiri ya matakwa yako. Ee Bwana.
3. Uwaokoe na hukumu zisizo za haki, wote wanaolitangaza jina lako na kuikiri
imani yao mbele ya watu wasiokujua Wewe. Ee Bwana.
4. Uamshe moyo wa sala ndani ya waamini wako, wapate kuongea nawe mara nyingi,
hasa wakati wa majaribu na majanga mbalimbali. Ee Bwana.
5. Uwapokee ndugu zetu marehemu wanaotamani kupata nafasi katika makao yako
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliye mwokozi na mlinzi wetu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.