ALHAMISI JUMA 33 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Mak.2:15-29
Watumishi wa mfalme waliokuwa wakiwashurutisha watu kuasi wakaja Modini kuwalazimisha hata Matathia
na wanawe walikuwapo. Watumishi wa mfalme wakamwambia Matathia, Wewe u kiongozi, mtu mkuu, maarufu
katika mji huu. Una wana wako na ndugu zako wa kujiweka upande wako. Basi, tangulia wewe, uitimize
amri ya mfalme, kama walivyofanya watu wote wa mataifa, na watu wa Uyahudi, nao waliosalia Yerusalemu.
Ndipo wewe na wana wako watahesabiwa kati ya rafiki za mfalme; naam, wewe na wana wako watatuzwa
fedha na dhahabu na vipawa vingi. Matathia akajibu, akasema kwa sauti kuu, Hata mataifa yote katika
milki ya mfalme wakimtii, wakiacha kila mtu dini ya wazee wake na kuchagua kuzifuata amri za mfalme,
lakini mimi sivyo. Mimi na wanangu na ndugu zangu tutaishika njia ya agano la baba zetu. Isiwe kwetu
kujitenga na sheria na maagano, hasha! Sisi hatutaisikiliza amri ya mfalme tugeuke katika dini yetu,
kwa kuume wala kwa kushoto. Alipokwisha kusema hayo, Myahudi mmoja alijitokeza machoni pa watu wote
kusudi atoe dhabihu juu ya madhabahu iliyokuwapo Modini, kama ilivyoamriwa na mfalme. Matathia
alipomwona, alishikwa na uharara, moyo wake ukatetemeka. Hasira yake ikatokeza hukumu, akamwendea
mbio, akamwua pale madhabahuni. Kisha alimwua yule mtu wa mfalme naye, aliyekuwa akiishurutisha
dhabihu, akaiangusha madhabahu. Hivyo alionyesha juhudi yake kwa sheria, kama juhudi ya Finehasi
juu ya Zimri, mwana wa Salu. Kisha, Matathia alipiga mbiu mjini kwa sauti kuu, akisema, Kila aliye
na juhusi kwa ajili ya sheria na kutaka kulitetea agano, na anifuate! Naye na wana wake wakakimbilia
milimani, wakiviacha vyote walivyokuwa navyo mjini. Ndipo wengi waliokuwa wakitafuta haki na hukumu
walikwenda jangwani wafanye maskani yao huko.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.50:1-2,5-6,14-15 (K)23
1. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
Toka maawio ya jua hata machweo yake.
Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri,
Mungu amemulika.
(K) Nitawaonyesha wokovu wa Mungu.
2. Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
Waliofanya agano nami kwwa dhabihu.
Na mbingu zitatangaza haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu. (K)
3. Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru,
Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
Ukaniite siku ya mateso;
Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. (K)
SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema: Mimi ndimi njia, na ukweli,
na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!
INJILI: Lk.19:41-44
Yesu alipofika karibu ya Yerusalemu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata
wewe, katika siku hii, yapasayo Amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku
zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande
zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa
sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu Wapendwa, katika siku yake Yerusalemu hakuyajua yapasayo amani. Kwa vile sisi
tunahitaji neema ya Mungu, tuombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wetu wa Kanisa wazidi kuhubiri amani na ulinzi wa imani yetu ya
kweli. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka serikalini wajaliwe busara na utu wema, wapate kutatua kwa
njia za haki na amani migogoro yote inayowakera raia wao. Ee Bwana.
3. Utujalie kuzishika kiaminifu mila njema za wazee wetu, tupate kuiiga imani
yao kwako na kuitetea mpaka mwisho. Ee Bwana.
4. Ekaristi Takatifu ituimarishe katika kumjua na kumpenda Kristo Mwanao,
aliyechinjwa sadaka kwa ajili ya watu wa dunia nzima; na akawafanya kuwa
ufalme na makuhani kwako. Ee Bwana.
5. Marehemu wanaongojea huruma yako waipate na kukaribishwa kwako mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tukupende Wewe zaidi ya chochote uyapokee maombi yetu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu Amina.