ALHAMISI JUMA 32 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Hek.7:22-8:1
Mradi ndani yake mna roho ya welekevu, takatifu, ya pekee, yenye namna mbalimbali, iliyoerevuka,
nyepesi kuenea, Dhahiri kusema, safi, wazi, isiyoharibika, ya kupenda wema, hodari, bila kuzuiwa,
yenye ukarimu, ya kupenda wanadamu, thabiti, amini, bila mashaka, yenye nguvu, yenye kuangalia mambo
yote, na kuingiliana na roho zote zilizo na welekevu, zilizo safi, zilizoerevuka sana. Kwa sababu
Hekima huenda upesi kila upande hata kupita mwendo wowote, naam, huenea kote kote katika mambo
yote na kupenya ndani yake kwa ajili ya usafi wake. Maana ndiyo pumzi ya uwezo wa Mungu, na miminiko
nakawa la utukufu wake Mwenyezi, hivyo lolote lililo najisi haliwezi kuingia ndani yake. Ndiyo
mwangaza kutoka kwa nuru ya milele, na kioo kisicho na mawaa cha kutenda kwake Mungu, na mfano
wa wema wake. Nayo ni moja, ina uwezo wa kutenda yote; hujikalia, huweza kuhuisha yote; na tangu
kizazi hata kizazi huwaingilia roho takatifu, huwafanya wanadamu kuwa rafiki za Mungu na manabii;
maana Mungu humpenda yeye tu akaaye na Hekima. Marini kuliko jua. Hekima hupita makundi ya nyota;
ikilinganishwa na nuru, huonekana ya kuwa imezidi; mradi baada ya nuru ya mchana hufuata usiku,
bali juu ya Hekima hakuna ovu liishindalo. Hekima huenea kwa nguvu nyingi toka pembe hii hata
pembe hii ya dunia, na kuyaratibisha mambo yote kwa jinsi ya kufaa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:89-91,130,135,175 (K)89
1. Ee Bwana, neno lako lasimama,
Imara mbinguni hata milele.
Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi.
Umeiweka nchi, nayo inakaa.
(K) Ee Bwana, neno lako lasimama hata milele.
2. Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo,
Maana vitu vyote ni watumishi wako.
Kufafanusha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga. (K)
3. Umwangazie mtumishi wako uso wako,
Na kunifundisha amri zako.
Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu,
Na hukumu zako zinisaidie. (K)
SHANGILIO: Zab.119:135
Aleluya, aleluya!
Umwangazie mtumishi wako uso wako,
na kunifundisha amri zako.
Aleluya!
INJILI: Lk.17:20-25
Yesu alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, Ufalme
wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama,
ufalme wa Mungu umo ndani yenu. Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku
moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione. Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku!
Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate; kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu
chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku
yake. Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu Wapendwa, Hekima ni nafsi ya Mungu na hutenda
kazi kwa jinsi ya kufaa. Ee Mungu uliye Hekima itokayo
juu, twakuomba.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Ili viongozi wetu wa Kanisa wazidi kutufafanulia
ukweli kuhusu Hekima na ufalme wako ambao upo mioyoni mwetu. Ee Bwana.
2. Ili Hekima ambayo huenda kokote katika mambo yote
na kupenya ndani yake kwa ajili ya usafi wake, izuie
hila ya adui anayelipiga vita Kanisa lako. Ee Bwana.
3. Ili sisi sote tufanywe rafiki zako, Wewe Mungu, na
wa wajumbe unaowatuma kwetu, tupate kukaa na
Hekima. Ee Bwana.
4. Ili walezi katika shule zote wachukuliane kwa
upendo na wale wanaowalea; wakisisitiza uchaji
kwa Mungu, nidhamu, maadili mema, bidii katika
masomo na kazi za mikono. Ee Bwana.
5. Ili ndugu zetu marehemu wapate kuuona uso wako,
Wewe uliye Hekima ya milele. Ee Bwana.
Ee Mungu ambaye kwa hekima yako unaratibisha mambo
yote kwa jinsi ya kufaa, uyapokee maombi yetu. Kwa njia
ya Kristo Bwana wetu. Amina.