ALHAMISI JUMA 31 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Rum.14:7-12
Hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.27:1,4,13-14 (K)13
1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?

(K) Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA
Katika nchi ya walio hai.

2. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. (K)

3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai. Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
“Mimi ndimi nuru ya ulimwengu.
Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani,
bali atakuwa na nuru ya uzima.”
Aleluya!

INJILI: Lk.15:1-10
Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia Yesu wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Akawaambia mfano huu, akisema, Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aenda akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu. Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione? Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa vile kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele ya Mungu, tuombe neema yake.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Umjalie Askofu wetu F. ari ya kuendelea kuishi kwa ajili ya kundi alilokabidhiwa, na hivi kujikabidhi yeye mwenyewe kwako siku zote kama mali yako. Ee Bwana.

2. Uwakumbushe watu wa mataifa kuwa hakuna anayeishi au kufa kwa ajili yake mwenyewe, bali kwa ajili yako. Ee Bwana.

3. Utupe moyo wa huruma na mapendo ya kweli kwa wenzetu, na kutuamshia furaha pale wakosefu wanapotubu. Ee Bwana.

4. Utuongezee hamu ya kuipokea Ekaristi Takatifu; tupate kuonja daima furaha ya uwepo wako ndani yetu. Ee Bwana.

5. Utujalie kuyahesabu mambo yaliyo ya faida kwetu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo; na uwapokee marehemu wetu katika ufalme wako. Ee Bwana.

Ee Mungu ambaye Mwanao alikula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.