ALHAMISI JUMA 30 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Rum.8:31-39
Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.109:21-22,26-27,30-31 (K)26
1. Na Wewe, MUNGU, Bwana, unitendee kwa ajili ya jina lako, Kwa kuwa fadhili zako ni njema uniokoe. Kwa maana mimi ni mnyonge na mhitaji, Na moyo wangu umejeruhi ndani yangu.

(K) Ee Bwana, uniokoe sawasawa na fadhili zako.

2. Ee Bwana, Mungu wangu, unisaidie, Uniokoe sawasawa na fadhili zako. Nao wakajue ya kuwa ndio mkono wako; Wewe, Bwana, umeyafanya hayo. (K)

3. Nitamshukuru Bwana kwa kinywa changu, Naam, nitamsifu katikati ya mkutano. Maana atasimama mkono wa kuume wa mhitaji Amwokoe na wanaoihukumu nafsi yake. (K)

SHANGILIO: Zab.25:4,5
Aleluya, aleluya!
Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako.
Aleluya!

INJILI: Lk.13:31-35
Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka. Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa twaamini kuwa hakuna chochote kitakachotutenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu, tuombe tukisema:-

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwalinde Wachungaji wa Kanisa lako dhidi ya wote wenye nia mbaya na utume wao, ili waendelee kuutangaza ukweli wa Injili yako. Ee Bwana.

2. Viongozi wa serikali wazidi kuwa hodari na kukutegemea Wewe, Mungu, katika uweza na nguvu zako dhidi ya shetani na maadui wote; wavae silaha wapate kuwapigania watu wako. Ee Bwana.

3. Wote wanaohubiriwa habari za Mwanao waongoke na kumkiri, kwani ndiye “Mbarikiwa” ajaye kwa jina lako. Ee Bwana.

4. Utujalie imani thabiti kwako hata katika madhulumu, tukitumaini kuwa katika mambo hayo yote tutashinda, kwa jina la Mwanao Yesu Kristo aliyetupenda. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wakaribishwe kwenye makao yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.