ALHAMISI JUMA 29 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.6:19-23
Nasema kwa jinsi ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu. Kwa kuwa kama mlivyovitoa viungo
vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu vitumiwe na haki
mpate kutakaswa. Kwa maana mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na haki. Ni faida gani basi
mliyopata siku zile kwa mambo hayo mnayoyatahayarikia sasa? Kwa maana mwisho wa mambo hayo ni mauti.
Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida
yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele. Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali
karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.1:1-4,6 (K)Zab.40:5
1. Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.
2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
SHANGILIO: Yn.15:15
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema: Siwaiti tena watumwa, lakini ninyi nimewaita rafiki,
kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya!
INJILI: Lk.12:49-53
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni
nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata
utimizwe! Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali
mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu
kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti
yake, na binti na mamaye; mkwe na mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, kwa vile utakaso uliouratibisha ni faida ya
kuwekwa huru dhidi ya dhambi, twakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wetu wa Kanisa wawe tayari hata kufarakana
na mtu yeyote, kwa ajili ya kutetea ukweli
wa Injili yako na kumleta Kristo katika mazingira
yetu. Ee Bwana.
2. Ufungue mioyo ya wasioujua uhuru wa kweli, wapate
kujua kuwa mshahara wa dhambi ni mauti; bali
karama yako Mungu ni uzima wa milele. Ee Bwana.
3. Kwa kuwa miili yetu ni dhaifu, utujalie kuvitumia
viungo vyetu kwa njia za haki na adili, tupate
kutakatifuzwa. Ee Bwana.
4. Wenye shida za pekee wajaliwe wayatamaniyo kwa
kadiri ya utajiri wa utukufu wako; na wafanywe
imara katika imani na matumaini kwako. Ee
Bwana.
5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na kufunguliwa
milango ya mbinguni, wapate kuingia na
kuishi huko milele. Ee Bwana.
Ee Baba mwema, hayo yote tunayaomba kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.