ALHAMISI JUMA 28 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.3:21-30
Haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; ina shuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo
kwa njia ya Imani katika yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya
dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi
ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya Imani katika damu
yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote
zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye
kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu. Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya
namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya Imani. Basi, twaona ya kuwa mwanadamu
huhesabiwa haki kwa Imani pasipo matendo ya sheria. Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye
Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia; kama kwa kweli Mungu ni mmoja.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.130:1-6 (K)7
1. Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia,
Bwana, uisikie sauti yangu.
Masikio yako na yaisikilize,
Sauti ya dua zangu. (K)
(K) Kwa Bwana kuna fadhili na ukombozi mwingi.
2. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha,
Ili Wewe uogopwe. (K)
3. Nimemngoja Bwana, roho yangu imemngoja;
Na neno lake nimelitumainia.
Nafsi yangu inamngoja Bwana,
Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
Naam, walinzi waingojao asubuhi. (K)
SHANGILIO: Zab.119:28,33
Aleluya, aleluya!
Unitie nguvu sawasawa na neno lako,
Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya!
INJILI: Lk.11:47-54
Yesu aliwaambia wanasheria: Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio
waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea
maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao
watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika
tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya
madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wanasheria,
kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.
Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi,
wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, haki ya Mungu inashuhudiwa na Torati na
Manabii. Kwa vile wote wamefanya dhambi na
kupungukiwa na utukufu wa Mungu, tuombe:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Upokee Sadaka anayokutolea Askofu wetu F. na
Mapadre wote kwa niaba ya Mwanao Yesu Kristo,
ili kutupatanisha nawe katika damu yake kwa njia ya
imani. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za viongozi wetu wa serikali za
kudhibiti vitendo vya uhalifu, hasa umwagaji damu
isiyo na hatia, ili tuishi kwa amani na upendo.
3. Uwakinge watu wako na umwagaji wa damu isiyo na
hatia; ili wote wakutafutao kwa moyo mnyofu wapate
fursa ya kukuabudu bila hofu. Ee Bwana.
4. Ekaristi Takatifu tunayoipokea itupe nguvu na ujasiri
wa kukuabu na kuilinda imani yetu bila kufadhaishwa
na jambo lolote. Ee Bwana.
5. Uwajalie marehemu wetu uzima mpya pamoja na
watakatifu wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetuhesabia haki kwa imani, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.