ALHAMISI JUMA 27 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mal.3:13-20
Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako
kwa namna gani? Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo
yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi? Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio
walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao. Ndipo wale
waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho
kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake. Nao watakuwa
wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami
nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye. Ndipo mtakaporudi, nanyi
mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati yay eye amtumikiaye Mungu nay eye asiyemtumikia.
Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote
watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata
haitawaachia shina wala tawi. Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia,
lenye kuponya katika mbawa zake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.1:1-4,6 (K)Zab.40:4
1. Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.
2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
SHANGILIO: 1Pet.1:25
Aleluya, aleluya!
Pokeeni kwa upole neno la Mungu,
lililopandwa ndani,
liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya!
INJILI: Lk.11:5-13
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na
kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka
safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe;
mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?
Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha
kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake. Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni,
nanyi mtaona; bisheni, nayi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye
abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe?
Au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu
mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu
hao wamwombao?
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Bwana Mungu ambaye husikiliza
kilio cha wanaomcha. Ee Mungu, twakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wa Kanisa wajaliwe ujasiri wa kulihubiri
neno lako dhidi ya waovu, ili waamini wapate kuujua
ukweli na kukutumikia kwa moyo mnyofu. Ee Bwana.
2. Uwafunulie watawala dhalimu wa dunia lengo jema
la Wakristo; wapate kushirikiana nao katika
kusimamia sheria na taratibu zote zenye nia ya
kuleta haki, amani na usawa. Ee Bwana.
3. Uzuie kiburi na kishawishi cha kutafuta ishara, ili
wenye haki wapate kukutumikia na kuwaokoa
wengine. Ee Bwana.
4. Utujalie imani thabidi na bidii ya kusali bila kuchoka,
kwani Wewe ndiwe ujuaye wakati unaotufaa kwa
wokovu tunaoutarajia kwa jina lako. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wasihesabiwe makosa yao,
bali majina yao yaingizwe kwenye kundi la watakatifu
wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, Mwanao amesema aombaye hupewa. Basi,
utujalie hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.