ALHAMISI JUMA 25 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Hag.1:1-8
Katika mwaka wa pili wa Dario mfalme, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda na Yoshua, mwana wa Yeosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake Hagai nabii, kusema, Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, watu hawa husema, hu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujengwa nyumba ya Bwana. Ndipo neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa. Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka. Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.149:1-6,9 (K)4
1. Aleluya, Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Sifa zake katika kusanyiko la watauwa! Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya, Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao!

(K) Bwana awaridhia watu wake.

2. Na walisifu jina lake kwa kucheza, Kwa matari na kinubi wamwimbie! Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake, Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)

3. Watauwa na waushangilie utukufu, Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao. Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao, Na upanga mkali kuwili mikononi mwao. (K) 4. Kuwafanyia hukumu iliyoandikwa: Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. (K)

SHANGILIO: Zab.25:4,5
Aleluya, aleluya!
Unijulishe ee Bwana unifundishe mapito yako
Aleluya!

INJILI: Lk.9:7-9
Herode mfalme alisikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohane amefufuka katika wafu, na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Lakini Herode akasema, Yohane nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu anapenda kila jumuiya ya waamini iwe na mahali rasmi pa kukutana naye. Kwa vile mahali hapo ni mfano wa makao yake ya milele huko mbinguni, tusali tukisema:-

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ubariki juhudi za Askofu wetu F., ili kila jumuiya ya waamini ihamasike kuwa na nyumba bora ya ibada, upate kukutana nao humo kwa utulivu. Ee Bwana.

2. Viongozi wa serikali wajaliwe moyo wa ushirikiano na Wachungaji wetu katika kuleta hali bora ya maisha ya watu wako kimwili na kiroho. Ee Bwana.

3. Wabatizwa wote tuongezewe ari ya kulitii neno lako linalohubiriwa kwetu na Wachungaji uliowatuma kwetu badala yako. Ee Bwana.

4. Katika mkanganyo na ubatili wa mambo, utujalie kujikabidhi kwako ambako kuna maana ya mwisho na ya uhakika juu ya mambo yote. Ee Bwana.

5. Ndugu zetu marehemu wapate ufufuo na uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka tuushuhudie ukweli, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.