ALHAMISI JUMA 24 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Tim.4:12-16
Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo,
na katika upendo na imani na usafi. Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na
kufundisha. Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa
mikono ya wazee. Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote.
Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa
nafsi yako na wale wakusikiao pia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.111:7-10 (K)2
1. Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,
Maagizo yake yote ni amini,
Yamethibitika milele na milele,
Yamefanywa katika kweli na adili.
(K) Matendo ya Bwana ni makuu.
2. Amewapelekea watu wake ukombozi,
Ameamuru agano lake liwe la milele,
Jina lake ni takatifu la kuogopwa. (K)
3. Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima,
Wote wafanyao hayo wana akili njema,
Sifa zake zakaa milele. (K)
SHANGILIO: Zab.119:11
Aleluya, aleluya!
Nimeshika neno lako moyoni mwangu,
nisije nikakukosea.
Aleluya!
INJILI: Lk.7:36-50
Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika Yesu ale chakula kwake; akaingia katika nyumba yake
yule Farisayo, akaketi chakulani. Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi,
alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya
marimari yenye marhamu. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea
machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka
yale marhamu. Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu
kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya
kwamba ni mwenye dhambi. Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema,
Mwalimu, nena. Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia
tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika
hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe
nyingi. Akamwambia, Umeamua haki. Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke
huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi
miguu yangu; na hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu
amenipaka miguu yangu marhamu. Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni
nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo. Kisha alimwambia
mwanamke, Umesamehewa dhambi zako. Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema
mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi? Akamwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa,
enenda zako kwa amani.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa vile sisi sote ni watenda kazi katika
shamba la Bwana, kwa imani tumpelekee Mungu maombi
yetu.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Maaskofu na Mapadre wetu wasiache kuitumia karama
ya unabii iliyomo ndani yao, ili wawe kielelezo
kwa waamini wao katika usemi na mwenendo, katika
upendo, na katika imani na usafi. Ee Bwana.
2. Viongozi wa serikali watoe fursa kwa waamini kukuabudu
Wewe Mungu, ili neno lako lipate kuenea na
kuziokoa nafsi za watu wako. Ee Bwana.
3. Utuongezee sisi sote imani katika ukuu wako na katika
uwezo wako wa kuponya roho na mwili. Ee Bwana.
4. Tunawaombea matajiri, ambao kwa neema ya
Mungu wamekuwa kama walivyo, ili wazitumie
karama walizopewa kwa kulisaidia Kanisa na wote
wenye shida. Ee Bwana.
5. Uziokoe roho za ndugu zetu marehemu, wapate kufika
huko mbinguni na kukusifu milele. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetupatia imani iletayo wokovu, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.