ALHAMISI JUMA 22 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kol.1:9-14
Tangu siku tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya
mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana,
mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu;
mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila
namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi
wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika
ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:2-6 (K)2
1. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
2. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
3. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)
SHANGILIO: 1Pet.1:25
Aleluya, aleluya!
Neno la Bwana hudumu hata milele,
na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya!
INJILI: Lk.5:1-11
Makutano walipomsonga Yesu wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya
ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka,
wanaosha nyavu zao. Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke
kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena,
alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simony akajibu
akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa
neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao
zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje
kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipona
hayo, alianguka magotini pa yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi,
Bwana. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi
wa samaki waliopata; na kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika
wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha
kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu wapendwa, Mungu Baba alituingiza katika ufalme
wa Mwana wa pendo lake kutoka nguvu za giza. Na hivi
tunamshukuru tukisema.
Kiitikio: Upokee shukrani zetu.
1. Kwa kuwa umelipatia Kanisa lako viongozi wa kuiendeleza
kazi ya Mwanao, ili tujipatie ukombozi, yaani msamaha wa
dhambi. Ee Bwana.
2. Kwa kuwa umeijalia nchi yetu watawala wenye
hekima na upendo na wanaohimiza haki, amani na
ushirikiano. Ee Bwana.
3. Kwa kuwa kwa kupewa mahitaji yao ya kimwili na
kiroho, watu wako wanapata fursa ya kuutambua ukuu
na utakatifu wako na kuongoka. Ee Bwana.
4. Kwa kuwa umetuachia Ekaristi Takatifu inayotupatia
saburi, uvumilivu, maarifa, furaha, amani na umoja. Ee Bwana.
5. Kwa kuwa ndugu zetu marehemu wanaombewa msamaha
na kupewa uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, uwe radhi kuzipokea hizi shukrani zetu
pamoja na nia zingine tulizonazo ambazo hatukuzitaja.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.