ALHAMISI JUMA 21 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: 1The.3:7-13
Ndugu, tulifarijiwa kwa habari zenu, katika msiba na dhiki yetu yote, kwa imani yenu. Kwa kuwa sasa twaishi, ikiwa ninyi mnasimama imara katika Bwana. Maana ni shukrani gani tuwezayo kumlipa Mungu kwa ajili yenu, kwa furaha ile yote tuliyoifurahia, kwa sababu yenu mbele za Mungu wetu; usiku na mchana tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuyatengeneza mapungufu ya imani yenu? Basi Mungu mwenyewe, Baba yetu, na Bwana wetu Yesu, atuongoze na kuwazidisha katika upendo, ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.90:3-4,12-14,17 (K)14
1. Wamrudisha mtu mavumbini,
Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku.

(K) Utushibishe kwa fadhili zako,
tutashangili ana kufurahi.

2. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana, urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako. (K)

3. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti,
Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe. (K)

SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema: Mimi ndimi njia,
na ukweli, na uzima; mtu haji kwa Baba,
ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!

INJILI: Mt.24:42–51
Yesu aliwambia wanafunzi wake: Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja. Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, huku tukimshukuru Mungu kwa wema wake, kwa imani tumwombe katika shida zetu tukisema:-

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwajalie Askofu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa kusimama imara, kukesha na kuomba kwa juhudi dhidi ya maadui wa imani yetu kwako. Ee Bwana.

2. Wote wenye madaraka, hasa waajiri, wajaliwe kuwapa watu wako riziki zao kwa wakati wake, ili mioyo yao iwe bila lawama yoyote. Ee Bwana.

3. Utuongoze na kutuzidisha katika upendo sisi kwa sisi, na kwa watu wote; na hivi kujipatia utakatifu mbele zako. Ee Bwana.

4. Tunakushukuru kwa ajili ya wote wanaojitolea kulitegemeza Kanisa lako; tunakuomba uwaweke miongoni mwa walioitwa kuingia katika ushirika wa Mwanao, Yesu Kristo. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na kushirikishwa karamu ya uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyetaka Ekaristi Takatifu iwe Sadaka ya Shukrani, upokee sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.