ALHAMISI JUMA 20 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Amu.11:29-39
Roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni. Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli, ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa. Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake. Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli. Kisha Yeftha akafika Mispa nyumbani kwake, na tazama, binti yake akamtokea kumlaki, na matari na machezo; naye alikuwa ni mwanawe pekee; hakuwa na mwingine, mwana wala binti, ila yeye. Ikawa alipomwona akayararua mavazi yake, akasema, Ole wangu! Mwanangu, umenitweza sana, nawe u mmoja miongoni mwa hao wanisumbuao; kwa kuwa mimi nimemfunulia Bwana kinywa changu, nami siwezi kurejea nyuma. Binti yake akamwambia, Baba yangu, wewe umemfunulia Bwana kinywa chako; basi unifanyie sawasawa na hayo yaliyotoka kinywani mwako; kwa kuwa yeye Bwana amekulipia kisasi juu ya adui zako, hao wana wa Amoni. Kisha akamwambia baba yake, Basi na nifanyiwe neno hili; niache peke yangu muda wa miezi miwili, ili nipate kwenenda milimani, na kuombolea uanawali wangu, mimi na wenzangu. Akamwambia, Haya, enda. Akampeleka mbali muda wa miezi miwili; naye akaenda zake, yeye na wenziwe, akauombolea uanawali wake huko milimani. Basi ikawa mwisho wa hiyo miezi miwili, akarudi kwa babaye, aliyemtenda sawasawa na ile nadhiri yake aliyokuwa ameiweka; naye alikuwa hajamjua mtu mume.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.40:4,6-9 (K)7,8
1. Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo.

(K) Tazama ee Bwana, nimekuja.
Kuyafanya mapenzi yako.

2. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka. Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (K)

3. (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,) Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)

Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)

SHANGILIO: Zab.119:135
Aleluya, aleluya!
Uniangazie uso wako kwa wema,
unifundishe masharti yako.
Aleluya!

INJILI: Mt.22:1-14
Yesu aliwaambia makuhani na makutano kwa mithali, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa waake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watumwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu, ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusi. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu mwaminifu unayetaka tutimize ahadi na viapo vinavyokubalika kwako, twakuomba:-

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Askofu wetu wa Jimbo na Mapadre wazidi kuhimiza miito mitakatifu, ili jimbo letu lipate Mapadre, Watawa na Makatekista wa kutosha. Ee Bwana.

2. Viongozi wetu wa serikali na wa vyama vya siasa wajaliwe kuzitoa ahadi na sera zinazotekelezeka, na wawe waaminifu katika kutekeleza wajibu zao kwa jamii na taifa. Ee Bwana.

3. Umjalie kila mtu kuuitikia wito wake kila siku bila kutoa udhuru; na waliouitikia waishi kadiri ya sheria, kanuni na desturi za wito husika. Ee Bwana.

4. Uwarudishe wakosefu; uwaondolee moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama; uwanyunyizie maji safi na kuwatakasa, wapate kuzishika hukumu zako na kuzitenda. Ee Bwana.

5. Ndugu zetu marehemu, walioitikia na kuiishi miito mitakatifu, wajaliwe tuzo la milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Tunaomba hayo yote kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.