ALHAMISI JUMA 19 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Yos.3:7-11,13-17
Bwana alimwambia Yoshua, Hivi leo nitaanza kukutukuza mbele ya Israeli wote, wapate kujua ya kuwa
mimi nitakuwa pamoja na wewe, kama nilivyokuwa pamoja na Musa. Nawe uwaamuru hao makuhani walichukuao
sanduku la agano, ukawaambie, Mtakapofika ukingo wa maji ya Yordani, simameni katika Yordani. Basi
Yoshua akawaambia wanu Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya Bwana, Mungu wenu. Yoshua akasema,
kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu, na ya kuwa hatakosa kuwatoa mbele yenu
Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na Mwamori, na Myebusi. Tazama, sanduku la
agano la Bwana wa dunia yote linavuka mbele yenu na kuingia Yordani. Itakuwa, wakati nyayo za
makuhani walichukao sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakaposimama katika maji ya Yordani,
hayo maji ya Yordani yatatindika, maji yale yashukayo kutoka juu; nayo yatasimama kama chuguu. Hata
ikawa, hao watu walipotoka katika hema zao, ili kuvuka Yordani, makuhani waliolichukua sanduku la
agano wakatangulia mbele ya watu, basi hao waliolichukua hilo sanduku walipofika Yordani, na nyayo
za makuhani waliolichukua sanduku zilipotiwa katika maji ya ukingoni, (maana Yordani hujaa hata kingo
zake na kufurika wakati wote wa mavuno,) ndipo hayo maji yaiiyoshuka kutoka juu yakasimama, yakainuka,
yakawa chuguu, mbali sana, huko Adamu, mji ule ulio karibu na Sarethani, na maji yale yaliyotelemkia
bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yakatindika kabisa; watu wakavuka kukabili Yeriko. Na hao
makuhani waliolichukua sanduku la agano la Bwana wakasikamama imara mahali pakavu katikati ya Yordani;
Israeli wote wakavuka katika nchi kavu, hata taifa lile lote likaisha kuvuka Yordani.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.114:1-6
1. Aleluya.
Israeli alipotoka Misri,
Na Yakobo katika watu wa lugha ya kigeni.
Yuda ilikuwa patakatifu pake,
Israeli milki yake.
(K) Aleluya.
2. Bahari iliona ikakimbia,
Yordani ilirudishwa nyuma.
Milima iliruka kama kondoo waume.
Vilima kama wana-kondoo. (K)
3. Ee bahari, una nini, ukimbie?
Yordani, urudi nyuma?
Enyi milima, mruke kama kondoo waume?
Enyi vilima, kama wana-kondoo? (K)
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu,
awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya!
INJILI: Mt.18:21–19:1
Petro alimwendea Yesu akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara
saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme
wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya,
aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe,
yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipowe ile deni. Basi yule mtumwa
akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule
akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake
akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka,
akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka,
walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita
akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa
kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa
watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi,
msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake. Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo, akatoka Galilaya
akafika mipaka ya Uyahudi, ng’ambo ya Yordani.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu ni mwenye huruma na anataka sisi
tuwe na huruma kama yeye. Tumwombe neema yake:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote
wa Kanisa hekima, kionjo na kipawa cha
upatanishi, ili amani ipate kutawala kati yetu na
duniani kote. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka wajaliwe kuchukua tahadhari
madhubuti dhidi ya majanga mbalimbali, ili kuulinda
uhai wa watu wako. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote moyo wa kusameheana bila masharti
wala kinyongo chochote. Ee Bwana.
4. Uwasaidie wakosefu kufungua macho na masikio
yao, wapate kuzisoma ishara za nyakati na kufanya
toba kwa wakati. Ee Bwana.
5. Uwarehemu wote wenye ulemavu na matatizo
mbalimbali; nao marehemu wetu wastarehe katika
amani yako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetuletea msamaha kwa upendo wako,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.