ALHAMISI JUMA 17 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.40:16-21,34-38
Musa alifanya hayo yote; kama yote Bwana aliyoagiza ndivyo alivyofanya. Hata mwezi wa kwanza wa
mwaka wa pili, siku ya kwanza ya mwezi, ile maskani ilisimamishwa. Musa akaisimamisha maskani,
akayaweka matako yake, akazisimamisha nguzo zake. Akaitanda hema juu ya maskani, akakitia kifuniko
cha hema juu yake; kama Bwana alivyomwamuru Musa. Akautwaa ule ushuhuda, akautia ndani ya sanduku,
akaiweka miti ya kuchukulia juu ya sanduku, akakiweka kiti cha rehema juu ya sanduku, kisha akalileta
sanduku akalitia ndani ya maskani, naye akalitundika pazia la sitara, akalisitiri sanduku la ushuhuda;
kama Bwana alivyomwamuru Musa. Ndipo lile wingu likaifunikiza hema ya kukutania, na huo utukufu wa
Bwana ukaijaza maskani. Wala Musa hakuweza kuliingia hema la kukutania, kwa sababu lile wingu
lilikaa juu yake, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani. Hapo lile wingu lilipoinuliwa kutoka
juu ya maskani, wana wa Israeli wakaenda mbele katika safari zao zote, bali kama lile wingu
halikuinuliwa, wakati ule hawakusafiri hata siku ile lilipoinuliwa tena. Kwa maana lile wingu la
Bwana lilikuwa juu ya maskani wakati wa mchana, na mlikuwa na moto ndani yake wakati wa usiku, mbele
ya macho ya nyumba ya Israeli katika safari zao zote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.84:2-5,7,10 (K)1
1. Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea,
Moyo wangu na mwili wangu
Vinamlilia Mungu aliye hai.
(K) Maskani zako zapendeza kama nini,
Ee Bwana wa majeshi.
2. Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kito,
Alipoweka makinda yake,
Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)
3. Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
Huendelea toka nguvu hata nguvu,
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu. (K)
4. Hakika siku moja katika nyua zako
Ni bora kuliko siku elfu.
Ningependa kuwa bawabu
Nyumbani mwa Mungu wangu. (K)
SHANGILIO: 1Pet.1:25
Aleluya, aleluya!
Neno la Bwana hudumu hata milele,
na neno hilo ni neno jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya!
INJILI: Mt.13:47-53
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini,
likakusanya wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema
vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika
watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko
kutakuwako kilio na kusaga meno. Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.
Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na
mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Ikawa Yesu alipoimaliza
mifano hiyo, alitoka akaenda zake.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu uliyewajia watu wako, ukaongea nao katika
hema, na kuwaongoza kwa mnara wa wingu, twakuomba.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Maaskofu na Mapadre wetu wasichoke kuwakutanisha
watu wako kanisani na kutolea Sadaka ya Ekaristi
Takatifu. Ee Bwana.
2. Uwe pamoja na Bunge letu pamoja na wote wanaotunga
na kuzisimamia sheria, ili wafanye yote kwa
niaba yako na kwa manufaa ya watu wako. Ee Bwana.
3. Kwa ajili ya wote wanaopuuzia masuala ya dini, ili
wakumbuke kuwa kama udongo unavyoweza
kufanyiwa lolote katika mkono wa mfinyanzi,
ndivyo tulivyo sisi wanadamu katika mkono wako.
Ee Bwana.
4. Umjalie kila mmoja wetu kujiandaa vema kwa siku
ya mwisho, ili huko mbinguni tukawekwe kwenye
kundi la wema. Ee Bwana.
5. Uzipokee roho za ndugu zetu marehemu na kuziingiza
katika ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, Wewe wayajua yote tunayopaswa kukuomba.
Utujalie hayo yote kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.