ALHAMISI JUMA 16 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.19:1-2,9-11,16-20
Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai.
Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli
wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako katika wingu
zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa
akamwambia Bwana hayo maneno ya watu. Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa; ukawatakase
leo na kesho: wakazifue nguo zao, wawe tavari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu Bwana atashuka
katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote. Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa
na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote
waliokuwa kituoni wakatetemeka. Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaltea ili waonane na
Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima. Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu
Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka
sana. Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti.
Bwana akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; Bwana akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa
akapanda juu.
WIMBO WA KATIKATI: Dan.3:52-56 (K)52
1. Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;
Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
(K) Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
2. Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;
Wastahili kusifika na kutukuzwa milele. (K)
3. Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)
4. Umehimidiwa utazamaye vilindi,
uketiye juu ya makerubi;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)
5. Umehimidiwa katika anga la mbinguni
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)
SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya!
Roho yangu inamngoja Bwana,
na neno lake nimeitumainia.
Aleluya!
INJILI: Mt.13:10–17
Wanafunzi walimwambia Yesu, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu akawaambia, Ninyi mmejaliwa
kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana yeyote mwenye kitu atapewa,
naye atazidishiwa tele; lakini yeyote asiye na kitu, hata kile alichonacho atanyang’anywa.
Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia
hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala
hamtaelewa; kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, na kwa
masikio yao hawasikii vema, na macho yao wameyafumba; wasije wakaona kwa macho yao, wakasikia
kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa
kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na
wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Yesu umesema: Yeyote mwenye kitu atapewa, naye
atazidishiwa tele. Ndiyo kusema msaada wa Mungu
unahitaji ushirikiano wa mlengwa. Basi tunakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwe pamoja na Papa wetu F.
na Askofu wetu F.
pamoja na viongozi wote wa Kanisa katika kazi ya
kulichunga kundi lako hapa duniani. Ee Bwana.
2. Ulegeze mioyo ya watawala wasiotaka kulisikia neno
lako; ili walao raia wao walisikie neno hilo na,
wakiisha kuamini, wakuongokee Wewe. Ee Bwana.
3. Upokee shukrani zetu kwa kuwa macho yetu yanaona
na masikio yetu yanasikia matendo yako makuu. Ee
Bwana.
4. Uwahurumie makuhani, wanasheria, wachungaji na
manabii wasiotimiza wajibu wao vizuri; na
uwarudishe katika njia iliyo sawa. Ee Bwana.
5. Uwajalie marehemu wetu kuuona uso wako mtukufu
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Yesu uliyejifumba katika Ekaristi Takatifu,
umetufunulia sisi mambo mengi ambayo manabii wengi na
wenye haki hawakuyaona wala kuyasikia. Tunakushukuru.
Unayeishi na kutawala milele na milele. Amina.