ALHAMISI JUMA 15 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Kut.3:13-20
Musa alimwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza. Jina lake n’nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, Mimi niko ambaye niko; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; Mimi niko amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote. Enenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri; Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misrei na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali. Nao watakusikia sauti yako; nawe utakwenda, wewe na wazee wa Israeli kwa mfalme wa Misri, na kumwambia, Bwana, Mungu wa Waebrania, amekutana nasi; basi sasa twakuomba, tupe ruhusa twende mwendo wa siku tatu jangwani, ili tumtolee dhabihu Bwana, Mungu wetu. Nami najua ya kuwa huyo mfalme wa Misri hatawapa ruhusa mwende zenu, la, hata kwa mkono wa nguvu. Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:1,5,8-9,24-27 (K)8
1. Aleluya. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake, Wajulisheni watu matendo yake. Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya, Miujiza yake na hukumu za kinywa chake.

(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.

2. Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilolifanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka. (K)

3. Akawajalia watu wake wazae sana, Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao. Akawageuza moyo wawachukie watu wake, Wakawatendea hila watumishi wake. (K)

SHANGILIO: Zab.19:8
Aleluya, aleluya!
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.
Aleluya!

INJILI: Mt.11:28-30
Yesu aliwaambia makutano: Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, Yesu anatuita kwake akisema: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Na tumwombe:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie. 1. Askofu wetu F. na mapadre wote wajaliwe kuziboresha mbinu za kichungaji, ili kurahisisha na kuimarisha uinjilishaji. Ee Bwana.

2. Wote wenye madaraka wajaliwe kuyatimiza kiaminifu majukumu yao ya kuikomboa jamii kutoka katika matatizo yanayowakera. Ee Bwana.

3. Uwaite vijana wengi kuingia miito ya upadre, utawa na ukatekista, ili Kanisa lako lipate watenda kazi wanaojitosheleza. Ee Bwana.

4. Uwarehemu watu wako, hasa wenye matatizo ya pekee, wanaokutafuta usiku na mchana, wapate kuyaona kwa wakati mwafaka matunda ya sala na kazi zao za kila siku. Ee Bwana.

5. Uwape uzima wa milele ndugu zetu marehemu uliowaita kwako. Ee Bwana.

Ee Mungu, unayetaka tujifunze upole na unyenyekevu wa Mwanao, tunakuletea maombi yetu haya. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.