ALHAMISI JUMA 14 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.44:18-21,23-29;45:1-5
Yuda alimkaribia Yusufu akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni
mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao. Wewe, bwana wangu
ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! mnaye baba, au ndugu? Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye
baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa
katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda. Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho
yangu yamwangalie. Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena. Ikawa
tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu. Kisha baba yetu
akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo
akiwapo pamoja nasi, tutashuka; maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa
pamoja nasi. Mtumwa wako, Baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alimzalia wana wawili;
mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo. Na mkiniondolea
huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu na msiba kaburini. Hapo Yusufu hakuweza kujizuia
mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu.
Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. Akapaza sauti yake akalia,
nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi
ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na
hofu mbele yake. Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema. mimi
ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi
zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha za watu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:16-21 (K)5
1. Bwana aliita njaa iijilie nchi,
akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu aliuzwa utumwani.
(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.
2. Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)
3. Mfalme alituma watu akamfungua,
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa Bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)
SHANGILIO: Ebr.4:12
Aleluya, aleluya!
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu,
li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya!
INJILI: Mt.10:7-15
Yesu aliwaambia mitume wake: Katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni
umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure,
toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari,
wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake. Na mji wo wote
au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata
mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na
iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala
kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni
mwenu. Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya
hukumu, kuliko mji ule.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu anazo njia nyingi za kuufanikisha mpango
wake wa ukombozi. Kwa imani na matumaini, tumwombe.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umjalie Askofu wetu F. uvumilivu
katika kuzikabili changamoto za sasa za kitume kwa ajili
ya ustawi wa jimbo letu. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wayatumie vyema madaraka
yao, ili kujenga jamii zenye haki, amani na
upendo wa kweli. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kutimiza wajibu zetu za kitume kwa
ujasiri na bila kutarajia malipo yoyote hapa duniani.
Ee Bwana.
4. Kwa huruma yako, patiliza ukali wa hasira yako
kwa wakosefu, maana Wewe ndiwe Mtakatifu
katikati yetu. Ee Bwana.
5. Uwapoze wagonjwa wetu, uwatakase wenye ukoma,
uwafukuze pepo wabaya na kuwafufua wafu kwa
uzima wa milele. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetujia kwa namna ya pekee kila
tunapoadhimisha Ekaristi Takatifu, uyapokee maombi
yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.