ALHAMISI JUMA 11 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 2Kor.11:1-11
Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami. Maana nawaonea wivu,
wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. Lakini nachelea; kama
yule nyoka alivyomdanganya hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi
kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho
nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye! Maana nadhani
ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nacho mitume walio wakuu. Lakini nijapokuwa mimi ni mtu
asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila neno tumedhihirishwa kwenu. Je!
Nalifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila
ujira? Naliwanyang’anya makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho langu ili niwahudumie ninyi. Nami
nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia
walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote nalijilinda nafsi yangu nisiwalemee hata
kidogo; tena nitajilinda. Kama vile vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu atakayenifumba
kinywa katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya. Kwa nini? Je! Ni kwa sababu siwapendi ninyi?
Mungu anajua.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.111:1-4,7-8 (K)7
1. Aleluya.
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
(K) Matendo yako Bwana ni kweli na hukumu.
2. Matendo ya Bwana ni makuu,
Na haki yake yakaa milele.
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
Bwana ni mwenye fadhili na rehema. (K)
3. Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,
Maagizo yake yote ni amini,
Yamethibitika milele na milele,
Yamefanywa katika kweli na adili. (K)
SHANGILIO: 1The.2:13
Aleluya, aleluya!
Lipokeeni neno la Mungu,
siyo kama neno la wanadamu,
bali kama neno la Mungu.
Aleluya!
INJILI: Mt.6:7-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa;
maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na
hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba
yetu uliyembinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani
kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo
wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. Kwa maana mkiwasamehe watu
makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala
Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Bwana wetu Yesu Kristo ametufundisha kusali.
Tumshukuru na kumwomba Mungu Baba aliyemtuma
Mwanae kwetu sisi tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wa Kanisa wajengewe mazingira mazuri ya
utume wao, ili wazidi kuihubiri Injili bila vikwazo na
bila kuwa mzigo kwa waamini wao. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka wasiige wala kuruhusu mitindo
tofauti ya kigeni inayoenda kinyume cha utu, maadili
mema na haki za binadamu. Ee Bwana.
3. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu yatukumbushe
daima kusali, kulitafakari neno lako na kutoa huduma
kwa upendo. Ee Bwana.
4. Wabatizwa wote wajaliwe ujasiri wa kulihubiri
neno lako bila woga wowote, kama walivyofanya
manabii wako watakatifu. Ee Bwana.
5. Uwaponye wagonjwa, wafungwa wavumilie mateso
yao na ndugu zetu marehemu wapokelewe huko
mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetusamehe ili nasi tupate kuwasamehe
wenzetu, pokea sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu. Amina.