ALHAMISI JUMA LA 11 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Mungu 'lipojaza dunia
Viumbe vyenye uhai,
Na alipoibariki
Izae iongezeke,
Ng'ombe wal'ishi kw'amani
Na vitu vitambaavyo,
Na waliishi pamoja
Simba na wanakondoo.

Aliwapa nchi kubwa
Zisizokanyagwa bado,
Na mimea akawapa
Iwe ndo chao chakula;
Mungu 'lipoangalia
Alivyokuwa kaumba
Aliona yote sawa,
Yote ni mazuri sana.

Atukuzwe Mungu Baba,
Baba wa kila uhai,
Asifiwe wake Mwana,
Na Roho Mtakatifu;
Kwa uwezo wake Mungu
Vyote huishi, humudu,
Katika Yeye hukoma
Vitu vyote hutulia.

ANT. I: Bwana, waamini wako watashangilia watakapokuwa wanaingia nyumbani mwako.

Zab.132 Sifa ya Nyumba ya Mungu
Bwana Mungu atampa kiti cha Mfalme Daudi, baba yake (Lk.1:32)

I
Ee Mungu, mkumbuke Daudi*
na taabu zote alizopata.

Ukumbuke, Ee Mungu, ahadi aliyokutolea,*
nadhiri aliyokuwekea, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo:

kwamba hataingia nyumbani,*
au kulala kitandani mwake;

hatakubali kulala usingizi,*
wala kusinzia,

mpaka akupatie wewe Mungu mahali,*
makao yako, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo!

Huko Efrata tulisikia habari za Sanduku la Agano,*
tukalikuta katika mashamba ya Yearimu.

“Haya! Twende nyumbani kwa Mungu;*
tuabudu mbele ya kiti chake cha enzi!“

Uje Hekaluni, Ee Mungu, na Sanduku la Agano,*
ishara ya enzi yako, ukakae huko milele.

Makuhani wako wawe waadilifu daima;*
na waaminifu wako wapige vigelegele vya furaha!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana, waamini wako watashangilia watakapokuwa wanaingia nyumbani mwako.

ANT. II: Bwana amechagua Sion kuwa makazi yake.

II
Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,*
usimkatae huyo mfalme wako uliyemteua.

Ulimpa Daudi ahadi rasmi,*
ahadi thabiti ambayo hutaivunja:

"Nitamtawaza mzao wako kuwa mfalme,*
naye atatawala baada yako wewe.

Watoto wako wakishika agano langu,*
na kuzingatia maagizo ninayowapa,

hata watoto wao vile vile*
wataendelea kuwa wafalme mahali pako.“

Mungu ameuchagua mji wa Sion,*
ametaka uwe kikao chake:

"Hapa ndipo nitakapokaa milele,*
ndipo mahali nitakapotawalia.

Nitaujalia mji wa Sion mahitaji yake yote;*
nitawashibisha chakula maskini wake.

Nitawafanikisha makuhani wake katika kazi zao;*
humo waaminifu wangu watapiga vigelegele kwa furaha.

Humo nitamfanya mzao wa Daudi awe mfalme shujaa;*
nitautegemeza utawala wa mfalme wangu mteule,

nitawaaibisha kabisa adui zake;*
lakini utawala wake utastawi sana.”

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana amechagua Sion kuwa makazi yake.

ANT. III: Bwana amempa mamlaka, heshima na milki; na watu wote watamtumikia.

WIMBO: Ufu.11:17-18;12:10b-12a Hukumu ya Mungu
Bwana Mungu Mwenyezi,*
uliyeko na uliyekuwako!

Tunakushukuru,/
maana umetumia nguvu yako kuu*
ukaanza kutawala!

Watu wa mataifa waliwaka hasira,/
maana wakati wa ghadhabu yako umefika,*
wakati wa kuwahukumu wafu.

Ndio wakati wa kuwatuza*
watumishi wako manabii,

watu wako na wote wanaolitukuza jina lako,*
wakubwa kwa wadogo.

Sasa wokovu utokao kwa Mungu umefika!/
Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika.*
Na Masiha wake ameonesha mamlaka yake!

Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu,*
aliyesimama mbele ya Mungu

akiwashtaki usiku na mchana,*
sasa ametupwa nje.

Ndugu zetu wameshinda/
kwa damu ya Mwanakondoo*
na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza;

maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana,*
wakawa tayari kufa.

Kwa sababu hiyo furahini enyi mbingu*
na vyote vilivyomo ndani yenu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana amempa mamlaka, heshima na milki; na watu wote watamtumikia.

SOMO: 1 Pet.3:8-9
Mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikra moja; mnapaswa kupendana kidugu, kuwa wapole na wanyenyekevu ninyi kwa ninyi. Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana ninyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka.

KIITIKIZANO
K. Bwana alitulisha ngano bora. (W. Warudie)
K. Alitushibisha asali itokayo mwambani.
W. Alitulisha ngano bora.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Bwana amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.

MAOMBI
Kristo ni kuhani mkuu wa watu wake: katika yeye ndio tunakusanyika kutoa sala zetu kwa Baba yetu.
W. Baba, ututie moyo mpya.

Tunakushukuru kwa kutushirikisha katika kanisa lako:
- Utujalie imani thabiti, na uifanye imani hiyo iwe chanzo cha uzima kwa wengine. (W.)

Bwana, umbariki Papa wetu F...:
- twaomba imani yake idumu daima, ili aweze kuwaimarisha ndugu zake. (W.)

Uwarudishe kwako wakosefu:
- utujalie moyo mnyenyekevu na wa majuto. (W.)

Mwanao alionja taabu na dhiki ya kuwa mbali na nchi yake;
- uwakumbuke wale wanaolazimika kuishi mbali na familia zao, au mbali na nchi zao. (W.)

Uwajalie marehemu pumziko la milele:
- uwakusanye watu wako wote mbinguni. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tumwombe Baba, kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Jioni hii tunakutolea shukrani zetu, Ee Bwana: kwa huruma yako utusamehe dhambi zetu tulizotenda kwa sababu ya udhaifu wetu wa kibinadamu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.