ALHAMISI JUMA 10 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: 2Kor.3:15–4:1,3–6
Hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao. Lakini wakati wowote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa. Basi ‘Bwana’ ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho. Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei. Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu. Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.85:8–13 (K)9
1. Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake Amani,
Naam, na watauwa wake pia,
Bali wasiurudie upumbavu tena.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.

(K) Utukufu wake ukae katika nchi yetu.

2. Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na Amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)

3. Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zetu kuwa njia. (K)

SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
awape roho wa hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya!

INJILI: Mt.5:20-26
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu ambaye kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo, ametupatia Ekaristi Takatifu na wahudumu wake.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Baba Mtakatifu wetu F. na Maaskofu wote kuendelea kutoa miongozo ya msingi, yenye kuimarisha imani aliyotuachia Mwanao. Ee Bwana.

2. Viongozi wa kiraia washirikiane na viongozi wa dini nyakati zote; wakati wa raha na wakati wa taabu. Ee Bwana.

3. Uwaepushe wachungaji wetu wote na kishawishi cha kujihubiri wenyewe, badala ya kumhubiri Kristo aliyewatuma. Ee Bwana.

4. Sisi sote tujaliwe kukumbuka kuwa kwa Ubatizo tumekuwa washiriki wa unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo Mwanao, ili tukutumikie Wewe kwa uchaji. Ee Bwana.

5. Uwashirikishe sasa karamu ya uzima wa milele huko mbinguni ndugu zetu marehemu uliowapenda. Ee Bwana.

Tunaomba hayo yote kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.