Des 29 OKTAVA YA NOELI
MASOMO
SOMO 1: 1Yoh.2:3-11
Wapenzi, Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua Yesu, ikiwa tunashika amri zake, Yeye asemaye, Nimemjua,
wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika
huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake. Yeye asemaye ya
kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda. Wapenzi, siwaandikii
amri mpya, ila amri ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Na hiyo amri ya zamani ni neno lile mlilolisikia.
Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na yenu; kwa kuwa giza linapita na vile nuru ya kweli
imekwisha kung’aa. Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa. Yeye
ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu
katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.96:1-3,5-6
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote,
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake. (K)
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.
2. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku,
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake. (K)
3. Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu,
Heshima na adhama ziko mbele yake,
Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Siku takatifu imetung’aria:
Enyi mataifa, njoni mkamwabudu Bwana:
Kwa sababu mwanga mkubwa umeshuka duniani.
Aleluya.
INJILI: Lk.2:22-35
Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, walikwenda na Yesu hata Yerusalemu,
wamweke kwa Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana, wakatoe
na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale
Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki,
mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho
Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho;
na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe
alimpokea mkononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa Amani kama ulivyosema
kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,
na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Nababye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni
akawabariki akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli,
na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.
MAOMBI
Ndugu, Mungu ni Upendo na anataka tuwapende pia ndugu zetu kama yeye alivyotupenda sisi. Hii siyo kazi
rahisi. Tumwombe ili tupate kuyajibu vema mapendo yake kwetu sisi wanadamu.
Kiitikio: Mungu wa huruma utusikie.
1. Kuzaliwa kwa Mwanao kutuongezee fahari katika kushika amri zako.
2. Utujalie upendo wa kidugu, ili tuwe kweli watu wa mwanga na wafuasi halisi wa Mwanao aliyezaliwa
kati yetu, apate kuondoa giza la dhambi.
3. Uamshe ndani ya Waamini wako moyo wa kumtolea Mwanao sadaka safi kama walivyofanya Bikira Maria
na Yosefu Mtakatifu.
4. Watumishi wako waliokufani wajikabidhi kwako, wapate kushiriki wokovu uliowekwa tayari machoni
pa watu wote.
Ee Mungu, Mwanao aliwekwa kwa kuanguka na kuinuka kwa wengi na kuwa ishara ya kunenewa. Utujalie
unyenyekevu kama ule wa Bikira Maria, aliyekubali hata upanga umwingie moyoni mwake, yapate kufunuliwa
mawazo ya mioyo mingi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.