WATAKATIFU SIMONI NA YUDA MITUME
MASOMO
SOMO: Efe.2:19-22
Tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa
nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe
ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu
takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:1-4(K)4
1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa.
(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.
2. Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
Katika hizo ameliwekea jua hema. (K)
SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana.
Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:12-16
Yesu aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata
kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita
Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohane, na Filipo
na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa
Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti.
MAOMBI
Mungu amewafanya mitume kuwa mashahidi na watangazaji wa kwanza wa ufufuko wa Mwanae Yesu Kristo. Tumwombe Mungu ili kazi
ya kitume tuliyopewa kwa Ubatizo izae matunda ya wokovu.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ili Askofu wetu F. na wote walioirithi kazi ya mitume wako wazidi kuwa mfano bora wa umoja na upendo katika imani moja,
Bwana mmoja na Ubatizo mmoja. Ee Bwana.
2. Kwa maombezi ya Mt. Andrea mtume uwaamshie roho ya upendo, haki na amani duniani, wote wenye mamlaka katika serikali,
vyama vya siasa na jumuiya mbalimbali. Ee Bwana.
3. Ili waamini wote wasikie sauti yako inayowaita kuishi kadiri ya wito uliowaitia na waimarishwe katika kumshuhudia Kristo
kwa maneno na matendo mema. Ee Bwana.
4. Kwa ajili ya jumuiya (parokia) yetu, ili kwa kuumega mkate pamoja, na kwa mfano wa maisha yetu ya kitume, tukutukuze Wewe
Mungu na kuwavutia kwako ndugu zetu waliojitenga na Kanisa lako. Ee Bwana.
5. Ili, kwa sala za mitume wako, ndugu zetu marehemu F. wapokelewe katika ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Hayo tunayaomba kwako, Ee Mungu Baba, kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.