Oktoba 18
MTAKATIFU LUKA Mwinjili
IJUMAA JUMA LA 28 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.
Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.
Ee Mungu, hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.
ANT. I: Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, maana nimeamua kufuata
sheria zako.
Zab.119:169-176 XXII Kuomba msaada
Kilio changu kikufikie, Ee Mungu!*
Unipe maarifa kadiri ya ahadi yako.
Ombi langu likufikie;*
uniokoe kama ulivyoahidi.
Nitakutolea sifa kem kem,*
maana wanifundisha kanuni zako.
Nitaimba juu ya agizo lako,*
maana amri zako zote ni za haki.
Daima uwe tayari kunisaidia,*
maana nazifuata amri zako.
Natazamia sana uniokoe, Ee Mungu;*
sheria yako ndiyo furaha yangu.
Unijalie kuishi nipate kukusifu;*
na maagizo yako yanisaidie.
Natangatanga kama kondoo aliyepotea;/
uje kunitafuta miye mtumishi wako,*
maana sikusahau maagizo yako.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, maana nimeamua kufuata
sheria zako.
ANT. II: Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, chadumu milele.
Zab.45 Utenzi wa arusi ya kifalme
Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki (Mt.25:6)
I
Moyo wangu umejaa mawazo mema:/
namtungia mfalme shairi langu,*
ulimi wangu u tayari kama kalamu ya mwandishi mwepesi:
wewe u mzuri kuliko wanadamu wote,/
maneno yako ni fadhili tupu,*
naye Mungu amekubariki milele.
Ewe shujaa, weka upanga wako tayari;*
wewe ni mtukufu na mwenye fahari.
Songa mbele kwa ushindi, utetee haki na ukweli,*
mkono wako ukupatie ushindi mkubwa.
Mishale yako ni mikali,/
hupenya mioyo ya adui za mfalme;*
nayo mataifa huanguka chini yako.
Utawala wako ni kama wa Mungu, wadumu milele;*
wewe wawatawala watu wako kwa haki.
Wapenda uadilifu na kuchukia uovu./
Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuteua,*
na kukumiminia furaha kubwa zaidi kuliko wenzako.
Mavazi yako yanukia marashi na udi,/
wanamuziki wakuimbia katika majumba*
yaliyopambwa kwa pembe za ndovu.
Binti za wafalme ni baadhi ya wanaokulaki,/
naye malkia amesimama kulia kwako,*
amevaa mapambo ya dhahabu safi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, chadumu milele.
ANT. III: Niliona mji mpya, Yerusalemu, umepambwa kama bi arusi aliye
tayari kumlaki mumewe.
II
Nawe binti, sikiliza! Nisikilize kwa makini:*
sahau sasa watu wako na jamaa zako.
Uzuri wako wamvutia mfalme:*
yeye ni bwana wako, lazima umtii.
Watu wa Turo watakuletea zawadi;*
matajiri watataka upendeleo wako.
Binti mfalme anaingia - mzuri kabisa!*
Vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.
Amevalia vazi la rangi nyingi,*
aongozwa kwa mfalme
akisindikizwa na wanawali wenzake,*
nao pia wanapelekwa kwa mfalme.
Kwa furaha na shangwe wanafika huko,*
na kuingia katika jumba la mfalme.
Ee mfalme, utapata watoto wengi/
watakaotawala badala ya wazee wako;*
utawafanya watawale duniani kote.
Sifa zako nitazieneza kwa vizazi vyote daima,*
nayo mataifa yatakusifu daima na milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Niliona mji mpya, Yerusalemu, umepambwa kama bi arusi aliye
tayari kumlaki mumewe.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Rom.1:16-17
Mimi najiaminisha kabisa katika injili; yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini:
Wayahudi kwanza, na wasio Wayahudi pia. Kwa maana injili inaonesha wazi jinsi Mungu anavyowafanya
watu wawe na uhusiano mwema naye: jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho. Kama
ilivyoandikwa: "Mwenye uhusiano mwema na Mungu kwa imani, ataishi."
K. Sauti yao imeenea duniani kote.
W. Ujumbe wao umesikika kote ulimwenguni.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: 1Tes.2:2b-4
Ingawa kulikuwa na upinzani mwingi, Mungu wetu alitujalia uhodari wa kuwahubirieni Habari Njema
yake. Jambo tunalosisitiza kwenu si jambo linalotegemea uwongo au nia mbaya; wala hatupendi
kumdanganya mtu ye yote. Sisi twanena daima kama atakavyo Mungu, kwani yeye alituona kwamba
tunafaa, akatukabidhi hii Habari Njema. Si nia yetu kuwapendeza watu, hata kidogo, bali twataka
kumpendeza Mungu ambaye anajua mioyo yetu mpaka ndani.
K. Walifuata maagizo ya Mungu.
W. Walishika amri zake.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: 2Tim.1:8b-9
Shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unazopewa na Mungu. Yeye
alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya mastahili ya matendo yetu,
bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo kwa ajili ya Kristo Yesu
kabla ya nyakati.
K. Furahini na shangilieni.
W. Kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.
SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, ulimchagua Mtakatifu Luka, ili adhihirishe fumbo la upendo wako kwa maskini
kwa mahubiri na maandishi yake. Uwajalie wale ambao tayari wanakiri jina lako waendelee kuwa roho
moja na moyo mmoja, na hivyo mataifa yote yaweze kuona wokovu wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu
Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.