Generic placeholder image
Tarehe 29 Septemba

WAT. MIKAEL, GABRIEL NA RAFAEL MALAIKA
MASOMO

SOMO: Dan.7:9-10,13-14
Nilitazama viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; Kiti cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatokea ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadama akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zole, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.138:1-5 (K)1
1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako Takatifu,

(K) Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.

2. Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Kuliko jina lako lote.
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)

3. Ee Bwana wafalme wote wa dunia watakushukuru
Watakapo yasikia maneno ya kinywa chako.
Naam wataziimba njia za Bwana,
Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. (K)

SHANGILIO:Zab.103:21
Aleluya, aleluya!
Mhimidini Bwana enyi majeshi yake yote,
nanyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.
Aleluya!

INJILI: Yn.1:47-51
Yesu alipomwona Nathanael anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanael akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona. Nathanael akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli. Yesu akajibu, akamwambia, kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. Akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka Juu ya Mwana wa Adamu.

MAOMBI
Ndugu zangu, "Mungu amekuagizia malaika wake wakulinde katika njia zako zote." Tumwombe Mungu ulinzi wake kwa ujumbe wa malaika wake wakuu Mikael, Gariel na Rafael.

Ee Mungu wa majeshi,
1. Uwatume malaika wako walilinde Kanisa lako katika hatari zote.

2. Uwatume malaika wako wakinge nyumba zetu katika balaa na ajali.

3. Uwatume malaika wako wailinde nchi yetu, viongozi na raia wake.

4. Kwa nguvu ya Malaika Raphaeli utupe msaada katika matatizo yetu ya matibabu ya magonjwa ya kuambukiza.

5. Tunaomba malaika Michaeli atuimarishe katika mapamabano na nguzu za shetani.

6. Kwa msaada wa Malaika Gabrieli utupe nguvu ya kutimiza Neno lako tunalosoma katika maandiko matakatifu.

Ee Baba wa mbinguni, tunakuomba ulinzi wa malaika wako,tupate kusimama pamoja nao mbele ya uso wako milele. Kwa Kristo, Bwana wetu. Amina.