BIKIRA MARIA WA MATESO
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Lk.2:34-35
Simeoni akamwambia Maria: Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka kwa wengi walio katika Israeli,
na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako.
KOLEKTA:
Ee Mungu, ulitaka Mama wa mateso, asimame karibu na msalaba, ili ashiriki mateso ya Mwanao aliyetundikwa
msalabani. Ulijalie Kanisa lako, ili likiisha shirikishwa mateso yake Kristo, listahili kushiriki
ufufuko wake yeye, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Ebr.5:7-9
Kristo, siku hizo za mwili wake, alimtolea Yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi
na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni
Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu
ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.31:1-5,14-15,19 (K)16
1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
nisiabike milele kwa haki yako uniponye.
Unitegee sikio lako, uniokoe hima.
(K) Uniokoe, Ee Bwana, kwa ajili ya fadhili zako.
2. Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
nyumba yenye maboma ya kuniokoa,
ndiwe genge langu na ngome yangu
kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge. (K)
3. Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
maana wewe ndiwe ngome yangu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu,
umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)
4. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)
5. Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako
Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao
Mbele ya wanadamu! (K)
SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Bikira Maria anafurahi,
yeye ameshinda na kupata
nishani ya ushindi pasipo kufa,
alipokuwa chini ya msalaba wa Bwana.
Aleluya!
INJILI: Yn.19:25-27
Penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na
Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na Yule mwanafunzi aliyempenda amesimama
karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama,
mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.
Au:
Lk.2:33-35
Baba na mama wa Yesu walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki,
akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika
Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe
mawazo ya mioyo mingi.
MAOMBI
Ndugu zangu, Mama Maria alimtumikia Kristo kupita wote, ni mtakatifu kuliko wanawake wote.
Ee Baba mwema, kwa ajili ya mastahili ya Mama Maria usikilize maombi yetu:
1. Uwapatie watoto yatima makao na uwatulize wakimbizi.
2. Uwatulize na uwasaidie walioachwa na wenzao kwa sababu ya kifo.
3. Uwafariji wenye kuwaona wapenzi wao katika matata na mateso.
4. Uwape faraja wagonjwa wanaoteseka kwa magonjwa yasiyotibika.
5. Uwapokee kwako waliotuaga duniani na utukusanye kwako sisi wote pamoja na wapenzi wetu.
Ewe Mtakatifu, unakaa kusikopatikana sikitiko wala maumivu, kwa kuwa yapitayo yamekwisha pita.
Twakuomba, utupe msaada tunaposafiri katika njia ya machozi kama Mama wa Mkombozi na kufikia
heri na furaha isiyo na mwisho. Kwa Kristo, Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu mwenye huruma, upokee sala na dhabihu zetu tunazokutolea kwa sifa ya jina lako na kwa
heshima ya Bikira Maria mwenye heri ambaye, kwa wema wako, umetupatia awe mama yetu mwema,
aliposimama karibu na msalaba wa Yesu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI wa 1 wa Bikira Maria
ANTIFONA YA KOMUNYO: 1Pet.4:13
Kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa
shangwe.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumepokea sakramenti ya ukombozi wa milele. Tunakuomba kwa unyenyekevu ili tutimize
ndani yetu, kwa ajili ya Kanisa, yale ambayo yamepungua katika mateso ya Kristo, tukikumbuka
Bikira Maria mwenye heri alivyoshiriki mateso pamoja naye. Anayeishi na kutawala milele na milele.