KUZALIWA BIKIRA MARIA MTAKATIFU
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA:
Tusherehekee kwa shangwe kuzaliwa kwake Bikira Maria mtakatifu; kwake ametoka yule aliye jua la
haki, Kristo Mungu wetu.
Utukufu husemwa
KOLEKTA:
Ee Bwana, tunakuomba utupatie sisi watumishi wako zawadi ya neema ya mbinguni, ili wale ambao
uzazi wa Bikira Maria mtakatifu uliwaletea yule aliye chanzo cha wokovu, kwa sikukuu ya kuzaliwa
kwake huyo Bikira, wajaliwe ongezeko la amani. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao,
anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Mik.5:1-4
Bwana asema hivi: Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee binti wa vikosi; yeye ametuhusuru; watampiga
mwamuzi wa Israeli shavuni mwake kwa fimbo. Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni
mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye
matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele. Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati
wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli. Naye
atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao
watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia.
Au,
Rum.8:28-30
Twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema,
yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili
wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na
wale aliwachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale
aliowahesabia haki, hao akawatukuza.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.13:5-6 (K)Isa.61:10
1. Nami nimezitumainia fadhili zako;
Moyo wangu na uufurahie wokovu wako.
(K) Nitafurahi sana katika Bwana.
2. Naam, nimwimbie Bwana,
Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu. (K)
SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Ee Bikira Maria Mtakatifu,
umebarikiwa na unastahili sifa zote
kwa kuwa hua la haki,
Kristo Mungu wetu, amezaliwa na wewe.
Aleluya!
INJILI: Mt.1:1-16,18-23
Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka
akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake; Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi
akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu; Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni
akamzaa Salmoni; Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa
Yese; Yese akamzaa mfalme Daudi. Daudi akamzaa Sulemani kwa Yule mke wa Uria; Sulemani akamzaa
Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa
Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia;
Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia; Yosia akamzaa Yekonia na ndugu
zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli.
Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli;
Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori; Azori akamzaa Sadoki;
Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani;
Matani akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo.
Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi.
Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa
uwezo wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha,
aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika
ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa
uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye
atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana
kwa ujumbe wa nabii akisema,
Tazama bikira atachukua mimba,
Naye atazaa mwana;
Nao watamwita jina lake Imanueli;
Yaani, Mungu pamoja nasi.
MAOMBI
Ndugu wapendwa, leo tunaadhimisha sikukuu ya kuzaliwa Maria, Mama wa Kristo,
kiumbe kiteule. Tuombe.
Ee Bwana Mungu,
1. Utupe moyo wa mapendo kama Mama yetu Bikira Maria.
2. Utuepushe na dhambi za kujitenga nawe kama ulivyomkinga Bikira Maria na dhambi ya asili.
3. Kwa maombezi ya Bikira Maria aliye "Salama ya Wagonjwa." Uwasalimishe wagonjwa wa mwili na
wa roho.
4. Kwa sala za Bikira Maria "Kimbilio la wakosefu." Uwahurumie wakosefu wanaokukimbilia.
5. Kwa msaada wa Bikira Maria aliye "Msaada wa WaKristo." Uwasaidie waumini wote.
6. Kwa maombezi ya Mama Maria "Malkia wa Amani." Uyajalie mataifa yote amani na raha.
7. Kwa maombezi ya Mama Maria aliye "Malkia wa Ulimwengu." Utuopoe na matetemeko ya nchi,
mafuriko na majanga yote.
8. Utupokee kwako mbinguni ili tufurahi nawe na watakatifu wote.
Ee Baba wa mbinguni, twakushukuru kwa sababu mama wa Kristo ni mama yetu pia. Kwa ajili yake
utulinde kwa mapendo ya kibaba, tupate kukupendeza. Kwa Kristo, Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, ubinadamu wa Mwanao utusaidie, ili, yeye ambaye alipozaliwa na Bikira hakupunguza usafi
wa Mama, bali aliutakatifuza, kwa kutusamehe dhambi zetu, afanye dhabihu hii tunayokutolea
ikupendeze. Anayeishi na kutawala milele na milele.
Au:
Ee Bwana, tunakutolea vipaji vyetu tukiadhimisha kwa furaha kuzaliwa kwa Bikira Maria mtakatifu.
Tunakuomba kwa unyenyekevu ili, sisi tutiwe shime kwa ubinadamu wa Mwanao, aliyekubali kupata
mwili kwa huyo Bikira. Anayeishi na kutawala milele na milele.
UTANGULIZI wa 1 wa Bikira Maria
ANTIFONA YA KOMUNYO: Isa.7:14; Mt.1:21
Tazama, Bikira atamzaa Mwana, ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, Kanisa lako, ulilolifanya upya kwa mafumbo matakatifu, lishangilie linapofurahia kuzaliwa
kwake Bikira Maria mtakatifu, yeye ambaye amekuwa tumaini la ulimwengu mzima na pambazuko la
wokovu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.