KUNG'ARA SURA BWANA WETU YESU KRISTO
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Mit.17:5
Roho Mtakatifu alionekana katika wingu jeupe, na sauti ya Mungu Baba ikasikika ikisema: Huyu
ni Mwanangu, mpendwa wangu, niliyependezwa naye; msikieni yeye.
Utukufu husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, katika Mng'aro mtukufu wa Mwanao pekee ulithibitisha mafumbo ya imani kwa ushuhuda
wa mababu, na uliahidi kutufanya kikamilifu tuwe wanao wa urithi. Utujalie sisi watumishi wako
tuisikilize sauti ya Mwanao mpenzi na hivi tustahili kufanywa warithi pamoja naye. Anayeishi na
kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Dan.7:9-10,13-14
Mimi nilitazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi
yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha
enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita
mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake;
hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja
aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku,
wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote,
na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita
kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.97:1-2,5-6,9(K)1,9
1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
(K) Bwana ametamalaki, juu sana kuliko nchi yote.
2. Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake. (K)
3. Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu,
Juu sana kuliko nchi yote;
Umetukuka sana juu ya miungu yote. (K)
SOMO 2: 2Pet.1:16-19
Hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu
Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba
heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, huyu ni mwanangunu
mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa
pamoja naye katika mlima ule mtakatifu. Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo,
mkilianglia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na
nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.
SHANGILIO: Mt.17:5
Aleluya, aleluya!
Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu,
ninayependezwa naye,
msikieni yeye.
Aleluya!
INJILI MWAKA A: Mt.17:1-9
Yesu aliwatwaa Petro, na Yohane nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura
yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa
na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo
hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha
Eliya. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika
lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye. Na wale
wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana. Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni,
wala msiogope. Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani,
Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu yeyote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka
katika wafu.
INJILI MWAKA B: Mk.9:2-10
Yesu aliwatwaa Petro, Yakobo na Yohane, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao;
akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani
kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. Petro
akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja
chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa
na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu
ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu
pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu
waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu. Wakalishika neno lile,
wakiulizana wao kwa wao, Huko kufufuka katika wafu maana yake nini?
INJILI MWAKA C: Lk.9:28-36
Yesu aliwatwaa Petro na Yohane na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake
sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimetameta. Na tazama, watu wawili walikuwa
wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walionekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki
kwake atakakotimiza Yerusalemu.
Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka
waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. Ikawa hao walipokuwa wakijitenga
naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu;
kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo.
Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo.
Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye. Na sauti hiyo
ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lolote
katika hayo waliyoyaona.
Nasadiki husemwa: Ikiwa sikukuu hii inaangukia siku ya Dominika.
MAOMBI
Yesu aligeuka sura yake mbele ya wafuasi wachache na kuwaonesha utukufu wake wa mbinguni. Alitaka kuwaimarisha
na kuwatia moyo wa kumfuata katika njia ya mateso inayotustahilia tuzo ya mbinguni.
1. Ee Bwana Yesu, uliwaonesha wafuasi utukufu wa mbinguni. Utujalie alama za utukufu wako kwa kujaza mioyo
yetu furaha halisi ya kuteuliwa nawe.
2. Petro aligundua kwamba utukufu unatutamanisha tuwe nao daima. Utujaze hamu ya kutenda matendo yanayotuongoza
kwenye utukufu wa milele.
3. Katika mlima wa utukufu uliongea na wateule wa zamani. Utujalie hamu ya kuonja mambo ya mbinguni kwa
kuwasiliana na watakatifu wako.
4. Ee Bwana Yesu, Mungu Baba alikudhihirisha kuwa ndiwe Mwana wake wa pekee. Akatuambia: Msikieni yeye. Uzibue
masikio ya mioyo yetu ili tuwe tayari kukusikiliza wewe na wenzetu daima.
5. Uwashirikishe marehemu wetu utukufu wako.
Ee Mungu Baba, ni vigumu kutembea katika njia ya imani bila kuona miale michache ya mwanga wa utukufu. Utujalie
dalili chache kwa njia ya Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tuakuomba uvitakatifuze vipaji tunavyokutolea katika sikukuu takatifu ya kung'aa
sura Mwanao pekee. Nasi utusafishe madoa ya dhambi zetu kwa nuru ya mng'ao wake. Kwa njia
ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI: Fumbo la kung'ara Bwana wetu
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee
Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo, Bwana wetu.
Yeye aliuonesha utukufu wake mbele ya mashahidi aliowateua. Aliujaza mwili wake ulio sawa na
wengine kwa mng'ao mkubwa, ili kikwazo cha msalaba kiondolewe katika mioyo ya wafuasi wake.
Hivyo alionesha kuwa katika mwili wake Kanisa lote utatimia mng'ao uleule ambao uling'aa kwa
namna ya ajabu katika Kristo aliye kichwa chake.
Kwa hiyo, sisi pamoja na Nguvu za mbinguni, tunakutukuza daima hapa duniani tukisifu bila
mwisho adhama yako kwa sauti kuu:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.
ANTIFONA YA KOMUNYO: 1Yon.3:2
Bwana atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba, chakula cha mbinguni tulichokipokea kitubadilishe, ili tufanane na yeye
ambaye ulitaka kuudhihirisha utukufu wake alipong'aa sura. Anayeishi na kutawala milele na milele.