WAT. YOAKIM NA ANNA
MASOMO
SOMO: Ybs.44:1,10-15
Haya na tuwasifu watu wa utauwa, Na baba zetu katika vizazi vyao. Lakini hawa walikuwa watu wa
utauwa, wala kazi zao za haki hazisahauliki. Wema wao utawadumia wazao wao, Na urithi wao una
wana wa wana; Wazao wao wanashikamana na agano, Na watoto wao kwa ajili yao. Kumbukumbu lao
litadumu milele, Wala haki yao haifutiki kamwe; Miili yao imezikwa katika amani, Na jina lao
laishi hata vizazi vyote. Mkutano wa watu wataitangaza hekima yao, Na makusanyiko watazihubiri
sifa zao.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.132:11,13-14,17-18(K)Lk.1:32
1. Bwana amemwapia Daudi neno la kweli,
Hatarudi nyuma akalihalifu,
Baadhi ya wazao wa mwili wako
Nitawaweka katika kiti chako cha enzi.
(K) Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi,
baba yake.
2. Kwa kuwa Bwana ameichagua Sayuni,
Ameitamani akae ndani yake.
Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele,
Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani. (K)
3. Hapo nitamchipushia Daudi pembe,
Na taa nimemtengenezea masihi wangu.
Adui zake nitawavika aibu,
Bali juu yake taji yake itasitawi. (K)
SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Waliitarajia faraja ya Israeli,
na Roho Mtakatifu alikuwa juu yao.
Aleluya!
INJILI: Mt.13:16-17
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa
kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona
mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.
MAOMBI
Ndugu zangu, Mungu ametupenda akamtuma mwanaye Bwana Yesu Kristo ambaye alitupenda mpaka kufa
na kutupa amri kuu ya upendano. Tunaomba,
1. Kwa maombezi ya Watakatifu Yoakim na Anna uamshe ndani yetu hamu ya kukupenda wewe na kuwapenda
wenzetu kwa matendo.
2. Uwafanye watumishi wote wa Kanisa wawe wachungaji wanaowahurumia watu wanyonge hasa maskini
na wanaonewa.
3. Uwajaze waumini wote mioyo ya kuwa wajumbe wa upendo wako.
4. Uamshe ndani yetu moyo wa kuwa karibu na wagonjwa mahututi na wale wote walioachwa na jamaa
kuwasaidia.
5. Uwapelekee watoto yatima na wajane wajumbe wa upendo wako.
Ee Bwana Yesu ulisema: Mliyomtendea mmojawapo wa wadogo mmenitendea mimi. Kwa maombezi ya
Watakatifu Yoakim na Anna, utufungue macho yetu tuwaone wote wanaohitaji msaada wetu, unayeishi
na kutawala pamoja na Mungu Baba katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu daima na milele. Amina.