KUZALIWA KWA MT. YOHANE MBATIZAJI
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Yn.1:6-7: Lk.1:17
Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili
aishuhudie ile nuru, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.
Utukufu husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, ulimwinua mtakatifu Yohane Mbatizaji awaandae watu amini kwa ajili ya Kristo Bwana.
Uwajalie watu wako neema ya furaha za kiroho na uiongoze mioyo ya waamini wote katika njia ya
wokovu na amani. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika
umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.49:1-6
Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana
ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa
changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa
mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha. Akaniambia: Wewe u mtumishi wangu, Israeli,
ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu
bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na
sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo
tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya
Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi
wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; Zaidi ya hayo
nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.139:1-3,13-15(K)14
1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua,
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu,
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K) Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa.
Maana wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
2. Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
Matendo yako ni ya ajabu. (K)
3. Na nafsi yangu yajua sana,
Mifupa yangu haikusitirika kwako,
Nilipoumbwa kwa siri,
Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi. (K)
SOMO 2: Mdo.13:22-26
Paulo alisema, Mungu alimwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona
Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu Yote. Katika
uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohane
alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu Wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya Kuja
kwake. Naye Yohane alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi
siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya
miguu yake. Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu,
kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa.
SHANGILIO: Lk.1:76
Aleluya, aleluya!
Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu,
Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana
umtengenezee njia yake.
Aleluya!
INJILI: Lk.1:57-66,80
Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani
zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa
siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu
akasema, La, sivyo; bali ataitwa Yohane, Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye
jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba,
Jina lake ni Yohane. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia,
akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo
hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote walioyasikia wakayaweka
mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa
pamoja naye. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea
kwake kwa Israeli.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu zangu, Yoane Mbatizaji alimtayarishia Yesu njia, yaani, aliwatayarisha watu kumpokea Masia.
Tuombe.
Ee Baba wa mbinguni,
1. Uwaite vijana wawe tayari kuacha yote na kumtumikia Kristo.
2. Utupelekee watangulizi wanaowavuta watu kwa mahubiri na mifano yao.
3. Utusaidie sisi waumini wote kuwa mwanga kwa wote wasiomjua Kristo.
4. Utupe moyo wa kuwa tayari kujitolea kama watangulizi wa wengine kwa ajili ya Kristo.
5. Utujalie kumwona Kristo uso kwa uso siku ya kuitwa naye.
Ee Mungu Mwenyezi, utujulishe kushika kwa moyo wote njia aliyotuonesha Mtakatifu Yoane Mbatizaji.
Kwa Kristo, Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunavileta vipaji hivi altareni pako tunapoadhimisha kwa heshima kuzaliwa kwake
Yohane Mbatizaji, aliyetabiri ujio wa Mwokozi wa ulimwengu na akamtambulisha alipokuja. Anayeishi
na kutawala milele na milele.
UTANGULIZI: Utume wa Yohane Mbatizaji, Mtangulizi wa Bwana.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee
Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo, Bwana wetu.
Tunausifu ukuu wako katika mtakatifu Yohane, Mtangulizi wa huyo Mwanao, ambaye ulimpa heshima
ya kuwa mkubwa kati ya wazao Wa wanawake. Yeye alipozaliwa alileta furaha kubwa, na kabla ya
kuzaliwa aliushangilia ujio wa wokovu wa wanadamu. Ni yeye peke yake kati ya manabii wote
aliyemwonesha kwa watu Mwanakondoo aletaye ukombozi. Pia alimbatiza mwanzilishi mwenyewe wa
ubatizo, na kwa namna hiyo maji yanayotiririka yalitakatifuzwa. Hatimaye, kwa kumwaga damu
yake, alistahili kumtolea Yesu ushuhuda mkubwa kabisa.
Kwa hiyo, sisi pamoja na Nguvu za mbinguni, tunakutukuza daima hapa duniani tukisifu bila
mwisho adhama yako kwa sauti kuu:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Lk.1:78
Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, mwangaza utokao juu umetufikia.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumeshibishwa katika karamu ya Mwanakondoo wa Mungu. Tunakuomba ili Kanisa lako
linalofurahia kuzaliwa kwake mtakatifu Yohane Mbatizaji, aliyeutabiri ujio wake Yesu, limtambue
yeye aliye asili ya uzima mpya wa Kanisa. Anayeishi na kutawala milele na milele.