11 JUNI
MT. BARNABA MTUME
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina (aleluya).
UTENZI
Wote walo duniani
Wapaze zao sauti
Wakimuimbia sifa
Za ushindi za mbinguni
Yeye alowapatia
Mitume wake neema
Ya kupiga mbio zao
Tukufu ulimwenguni.
Kwalo neno lako wewe
Waliichukua nuru
Ya ukweli wa injili
Hadi kwenye upagani;
Utupatie na sisi
Nuru hiyo ya mbinguni
Macho yetu yafurahi
Na nyoyo zichangamke.
Kwa matakwa yako wewe
Uwezo walijaliwa
Wa kufunga, kufungua
Duniani na mbinguni;
Fungua nyororo zetu,
Twondolee dhambi zetu,
Katika mioyo yetu
Tia upya ne'ma yako.
Na kwa nguvu yako wewe
Walilitamka neno
Lililoponya magonjwa
Na afiya kurudisha;
Endeleza kwetu huo
Uwezowe wa kuponya,
Saidia wadhaifu
Imarisha wenye nguvu.
ANT. I: Ninyi ndio mlioambatana nami kiaminifu, katika majaribu
yangu, aleluya.
Zab.116:10-19 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Nilizidi kuamini hata niliposema:*
"Mimi naangamia.".
Hata niliposema kwa hofu,*
"Binadamu hawaaminiki."
Nimrudishie Mungu nini,*
kwa mema yote aliyonitendea?
Nitamtolea Mungu dhabihu ya kinywaji,*
nimheshimu kwa shukrani.
Nitamtimizia Mungu nadhiri zangu,*
mbele ya taifa lake lote.
Mungu huthamini kifo cha waaminifu wake.*
Ee Mungu, mimi ni mtumishi wako;
ni mtumishi wako kama alivyokuwa mama yangu,*
umeniweka huru.
Nitakutolea sadaka za shukrani,*
na kukupa heshima zangu.
Mbele ya taifa lako lote,/
ukumbini mwa Hekalu lako huko Yerusalemu,*
nitakutimizia yale niliyoahidi, Ee Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Ninyi ndio mlioambatana nami kiaminifu, katika majaribu
yangu, aleluya.
ANT. II: Mimi nipo kati yenu, aleluya.
Zab.126 Kuomba nguvu mpya
Mungu alipoturudisha tena Sion,*
tulikuwa kama wanaoota ndoto!
Hapo tuliangua kicheko;*
tulishangilia kwa furaha.
Nao watu wa mataifa mengine walisema:*
“Mungu amewatendea mambo makubwa!”
Kweli Mungu alitutendea maajabu,*
tulifurahi kweli kweli!
Ee Mungu, urekebishe tena hali yetu/
kama mvua inavyotiririsha maji*
katika mabonde makavu.
Wanaopanda kwa machozi*
watavuna kwa shangwe;
wanaokwenda kupanda mbegu huku wakilia,*
watarudi kwa furaha huku wakichukua mavuno.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Mimi nipo kati yenu, aleluya.
ANT. III: Sitawaiteni watumishi tena, nawaita rafiki zangu, kwasababu
nimewajulisheni kila kitu nilichosikia kwa Baba yangu, aleluya.
WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!
Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.
Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake
katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.
Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani
kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.
Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu
kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!
Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!
Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,
akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.
Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,
ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Sitawaiteni watumishi tena, nawaita rafiki zangu, kwasababu
nimewajulisheni kila kitu nilichosikia kwa Baba yangu, aleluya.
SOMO: Kol.1:3a-6
Daima tunamshukuru Mungu, Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea. Maana tumesikia
juu ya imani yenu katika Kristo Yesu, na juu ya mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu. Wakati ujumbe
ule wa kweli, yaani ile Habari Njema ilipowafikieni kwa mara ya kwanza, mlipata kusikia juu ya lile
tumaini linalopatikana kwake. Kwa sababu hiyo imani na mapendo yenu yanategemea jambo lile mnalotumainia,
ambalo mmewekewa salama mbinguni. Injili inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote, kama vile
ilivyofanya kwenu ninyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu, na kuitambua ilivyo kweli.
KIITIKIZANO Wakati Usio wa Pasaka
K. Utangazeni utukufu wa Bwana; utangazeni kwa mataifa. (W. Warudie)
K. Simulieni maajabu yake kwa watu wote.
W. Yatangazeni kwa mataifa.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utangazeni...
KIITIKIZANO Wakati wa Pasaka
K. Utangazeni utukufu wa Bwana; utangazeni kwa mataifa, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Simulieni maajabu yake kwa watu wote.
W. Aleluya, aleluya
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utangazeni...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu,
ambayo Mungu alikuwa ametenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine (aleluya).
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo
wakieleza miujiza na maajabu, ambayo Mungu alikuwa ametenda kwa mikono yao kati ya watu wa
mataifa mengine (aleluya).
MAOMBI
Ee Mungu, Baba wa nuru, kwa njia ya injili ya Mwanao ulitualika tushiriki imani ya kweli.
Tunakuomba sasa kwa ajili ya taifa lako teule, tukisema:
W. Ulikumbuke Kanisa lako, Ee Bwana.
Baba, ulimfufua Mwanao kutoka wafu, ili awe mchungaji wa kundi kubwa;
- utufanye sisi tuwe mashahidi wake hata miisho ya dunia. (W.)
Ulimtuma Mwanao ulimwenguni kuwatangazia maskini habari njema;
- utujalie tuweze kuifikisha injili yake kwenye giza la maisha ya watu. (W.)
Ulimtuma Mwanao kupanda mioyoni mwa watu mbegu ya uzima usioharibika;
- utuwezeshe kueneza neno lake, na kupata mavuno ya kufurahisha. (W.)
Ulimtuma Mwanao kuupatanisha ulimwengu nawe kwa kumwaga damu yake;
- utushirikishe kazi yake ya kuwafanya wanadamu wawe rafiki zako tena. (W.)
Ulimweka Mwanao upande wako wa kuume huko mbinguni;
- uwapokee marehemu katika furaha ya utawala wako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, ulimjaza Mtakatifu Barnaba imani na Roho Mtakatifu, na ukamteua afanye kazi ya kuwaongoa
watu wa mataifa mengine. Ujalie injili ya Kristo aliyoihubiri kwa bidii sana, itangazwe kiaminifu siku
hizi, kwa maneno na matendo. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na
kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.