11 JUNI
MT. BARNABA MTUME
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Roho Mtakatifu amesema kwa njia ya manabii na walimu wa Kanisa: njooni, tumwabudu (aleluya)
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI
Enyi baba wa imani-
Yetu ya kale imani,
Pamoja na anga zote
Twaziimba sifa zenu
Ambao sauti zenu
Lisikika duniani,
Kristo mkimtangaza,
Jina lake litukuza.
Maskini mliwapa
Habari Njema: Injili,
Neno la Mungu liwaka
Ndani mwenu lilimeta,
Na lahubiriwa tena
Siku hizi kwetu sisi,
Neno lisilozeeka,
Neno jipya siku zote.
Mlimtangaza Mungu
Alotufilia sisi,
Na akaacha mauti
Mshindi akafufuka,
Ukweli katupatia
Uliotufanya huru
Ndiye asobadilika
Karne hata karne.
Atukuzwe Baba, Mwana,
Na Roho Mtakatifu,
Katupatia imani,
Imani isiyokufa:
Ni nuru katika giza
Tangu sasa hadi hapo
Nyota ile ya mchana
Ichomozapo nyoyoni.
ANT. I: Hii ni amri yangu: pendaneni kama mimi nilivyowapenda
ninyi (aleluya).
Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.
Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.
Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.
Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.
Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.
Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.
Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.
Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;
maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.
Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Hii ni amri yangu: pendaneni kama mimi nilivyowapenda
ninyi (aleluya).
ANT. II: Mtu hawezi kuwa na upendo mkuu zaidi kuliko ule wa kuutoa
uhai wake kwa ajili ya rafiki zake (aleluya).
WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)
Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.
Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.
Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.
Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.
Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.
Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.
Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.
Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.
Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.
Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.
Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.
Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.
Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.
Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.
Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
ANT. II: Mtu hawezi kuwa na upendo mkuu zaidi kuliko ule wa kuutoa
uhai wake kwa ajili ya rafiki zake (aleluya).
ANT. III: Ninyi ni rafiki zangu mkitenda ninayowaamuru, asema
Bwana (aleluya).
Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo,
mfalme wao (Hesychius)
Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!
Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.
Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.
Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.
Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.
Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,
ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;
wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.
kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Ninyi ni rafiki zangu mkitenda ninayowaamuru, asema
Bwana (aleluya).
SOMO: 1Kor.15:1-2a,3-4
Ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni, nanyi mkaipokea na kusimama
imara ndani yake, na kwa njia yake mnaokolewa. Mimi niliwakabidhi ninyi mambo muhimu sana ambayo
mimi niliyapokea: kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kufuatana na maandiko matakatifu;
kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kama ilivyoandikwa.
KIITIKIZANO Wakati usio wa Pasaka
K. Walisimulia matukufu ya Bwana, na matendo yake ya enzi. (W. Warudie)
K. Waliongelea matendo ya ajabu aliyokuwa amefanya.
W. Matendo yake ya enzi.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Walisimulia...
KIITIKIZANO Wakati wa Pasaka
K. Walisimulia matukufu ya Bwana, na matendo yake ya enzi, aleluya, aleluya.(W. Warudie)
K. Waliongelea matendo ya ajabu aliyokuwa amefanya.
W. Aleluya, aleluya
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Walisimulia...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Kisha Barnaba alienda Tarso kumtafuta Saulo. Alipompata alimpeleka Antiokia. Nao wote wawili
walikaa katika Kanisa la Antiokia, wakafundisha watu wengi (aleluya).
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Kisha Barnaba alienda Tarso kumtafuta Saulo. Alipompata alimpeleka
Antiokia. Nao wote wawili walikaa katika Kanisa la Antiokia, wakafundisha watu wengi (aleluya).
MAOMBI
Mwokozi wetu aliyaangamiza mauti, na kwa njia ya injili ametufunulia uzima wa milele. Kwa furaha
na shangwe, tumtangaze tukisema:
W. Uliimarishe Kanisa lako katika imani na mapendo.
Bwana Yesu, zamani uliliongoza taifa lako kwa njia ya watu watakatifu na wenye hekima;
- uwawezeshe Wakristo kufurahia daima ishara hii ya upendo wako mkuu. (W.)
Uliwasamehe watu wako dhambi zao walipoombewa na wachungaji watakatifu;
- kwa maombezi yao yenye nguvu, uendelee kulitakasa Kanisa lako. (W.)
Walipokuwa pamoja na ndugu zao, uliwateua hao watakatifu wako, na ukawashushia Roho wako;
- uwajaze Roho wako Mtakatifu viongozi wote wa taifa lako. (W.)
Hakuna kilichoweza kuwatenganisha wachungaji watakatifu na upendo wako;
- usimpoteze hata mmoja kati ya hao uliowakomboa kwa mateso yako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, ulimjaza Mtakatifu Barnaba imani na Roho Mtakatifu, na ukamteua afanye kazi ya kuwaongoa
watu wa mataifa mengine. Ujalie injili ya Kristo aliyoihubiri kwa bidii sana, itangazwe kiaminifu siku
hizi, kwa maneno na matendo. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na
kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.