MT. BARNABA MTUME
MASOMO
SOMO: Mdo.11:21-26,13:1-3
Watu wengi waliamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa
lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika
na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote wawaambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana
alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na Imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kisha
akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda
wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa
Wakristo kwanza hapo Antiokia. Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na
waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu
wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga,
Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga
na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-6(K)2
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa.
2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
4. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)
SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Ee Mungu, tunakusifu,
tunakukiri kuwa Bwana.
Jamii tukufu ya mitume inakusifu.
Aleluya!
INJILI: Mt.10:7-13
Yesu aliwaambia mitume wake, Katika kuenenda kwenu, hubirini , mkisema, Ufalme wa mbinguni
umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure,
toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari,
wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake. Na mji wowote
au kijiji chochote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata
mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na
iifikilie; ya, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.
MAOMBI
Ndugu zangu wapendwa, Kwa maombezi ya Mitume tumwombe Kristo, Bwana wa Kanisa lake.
1. Uliwaweka mitume kuwa mashahidi wa ufufuko wako na kuwatuma duniani kote waitangaze habari
hii ya furaha: Uwasaidie Baba Mtakatifu J. na maaskofu wote uliowachagua
kuwa mahalifa wa mitumne wako kuliongoza kanisa lako kwa busara na hekima.
2. Uliwaagiza mitume watangaze neno lako kati ya mataifa yote: Uwajaze Roho Mtakatifu wahubiri
wote wa neno lako.
3. Uliweka kanisa lako juu ya msingi wa mitume: Ulifanye Kanisa lako kuwa alama ya umoja na ya
amani kati ya mataifa.
4. Uliwaagiza mitume wawaondolee dhambi wale wote wanaotubu: Uwatie moyo mpya wote wanaoungama
dhambi zao.
Bwana Yesu, unastahili kupokea heshima yote, upokee shukrani na sifa katika Kanisa lako pamoja
na Baba na Roho Mtakatifu sasa na siku zote daima na milele. Amina.