Generic placeholder image

MTAKATIFU KAROLI LWANGA na WENZAKE
Wafiadini
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana wetu alipita
Ile njia ya mateso,
Na kwa kuwa yake damu
Kamwaga kwa 'jili yetu,
Inafaa sisi watu
Tutoe uhai wetu
Kwa ajili yake Mungu
Alotupa. Aleluya!

Si aibu kumwungama
Mwokozi msulibiwa!
Yeye ni uhai wetu
Usio wala na mwisho;
Si aibu kumwungama
Mungu wetu alokufa,
Pia kwa ajili yake
Sisi kufa. Aleluya!

Taji akiitazama
Milele alowekewa,
Mfyadini ajitia
Mikononi mwa mauti;
Kwa kufa kuyapindua,
Mauti anayashinda;
Adui huwapindua,
Huwashinda. Aleluya!

Bwana utufanye tuwe
Askari wako bora;
Tupe imani thabiti,
Tujalie roho safi;
Tuweze kuvumilia-
Mbele ya msalabao -
kwa ajili ya jinalo
Jina lako. Aleluya.

ANT. I: Miili ya watakatifu imezikwa katika amani, na majina yao huendelea kukumbukwa na vizazi vyote (aleluya).

Zab.116:1-9 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Nampenda Mungu, kwa maana anisikia,*
maana amesikiliza kilio cha ombi langu.

Yeye hunisikiliza*
kila ninapomlilia.

Hatari ya kifo ilinizunguka,/.
vitisho vya kaburi vilinivamia;*
nilijawa mahangaiko na majonzi.

Kisha nikamlilia Mungu:*
“Ee Mungu, tafadhali unisalimishe!“

Mungu amejaa wema na haki;*
Mungu wetu ni mwenye huruma.

Mungu huwalinda wanyofu;*
nilikuwa nimekandamizwa, naye akaniokoa.

Uwe na utulivu mkuu, ee roho yangu,*
kwa maana Mungu amenitendea vyema.

Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;*
akanilinda nisije nikaanguka.

Basi, nitatembea mbele yake Mungu,*
katika nchi ya watu walio hai.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Miili ya watakatifu imezikwa katika amani, na majina yao huendelea kukumbukwa na vizazi vyote (aleluya).

ANT. II: Niliziona roho za wote waliokuwa wameuawa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu, na kwa sababu ya kulihubiri neno la Mungu (aleluya).

Zab.116:10-19 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Nilizidi kuamini hata niliposema:*
"Mimi naangamia."

Hata niliposema kwa hofu;*
"Binadamu hawaaminiki."

Nimrudishie Mungu nini,*
kwa mema yote aliyonitendea?

Nitamtolea Mungu dhabihu ya kinywaji,*
nimheshimu kwa shukrani.

Nitamtimizia Mungu nadhiri zangu,*
mbele ya taifa lake lote.

Mungu huthamini kifo cha waaminifu wake.*
Ee Mungu, mimi ni mtumishi wako;

ni mtumishi wako kama alivyokuwa mama yangu;*
umeniweka huru.

Nitakutolea sadaka za shukrani,*
na kukupa heshima zangu.

Mbele ya taifa lako lote,/
ukumbini mwa Hekalu lako huko Yerusalemu,*
nitakutimizia yale niliyoahidi, Ee Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Niliziona roho za wote waliokuwa wameuawa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu, na kwa sababu ya kulihubiri neno la Mungu (aleluya).

ANT. III: Hawa ndio watakatifu waliotoa ushuhuda juu ya Mungu, kwa kuyatelekeza kando maisha ya kidunia. Wameyatakasa mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo (aleluya).

WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12
Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
unastahili utukufu na heshima na nguvu;

maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako*
kila kitu kimepewa uhai na uzima.

Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,

kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.

Mwana-kondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea

uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Hawa ndio watakatifu waliotoa ushuhuda juu ya Mungu, kwa kuyatelekeza kando maisha ya kidunia. Wameyatakasa mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo (aleluya).

------------------------
WAKATI USIO WA PASAKA
SOMO: 1Pet.4:13-14

Furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo, ili mweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa. Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa juu yetu.

KIITIKIZANO
K. Furahini katika Bwana. Wenye haki na washangilie kwa furaha. (W. Warudie)
K. Waadilifu na waimbe sifa.
W. Wenye haki na washangilie kwa furaha.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Furahini...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Watakatifu waliofuata nyayo za Kristo, wanafurahi mbinguni. Walitoa uhai wao kwa ajili ya upendo wao kwa Kristo; kwa hiyo watatawala milele pamoja naye.

------------------------
WAKATI WA PASAKA
SOMO: Ufu.7:14-17

Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwana-kondoo, yakawa meupe kabisa. Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda. Hawataona tena njaa wala kiu, jua wala joto kali halitawachoma tena, kwa sababu Mwana-kondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.

KIITIKIZANO
K. Waadilifu watang'aa mbele ya Mungu, aleluya, aleluya.(W. Warudie)
K. Walio na moyo safi watafurahi
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Waadilifu...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Furahini, enyi watakatifu, mbele ya Mwana-kondoo; ufalme ulitayarishwa kwa ajili yenu tangu mwanzo wa ulimwengu, aleluya.

------------------------
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Kipindi kawaida
Watakatifu waliofuata nyayo za Kristo, wanafurahi mbinguni. Walitoa uhai wao kwa ajili ya upendo wao kwa Kristo; kwa hiyo watatawala milele pamoja naye.

Ant. Kipindi cha Pasaka
Furahini, enyi watakatifu, mbele ya Mwana-kondoo; ufalme ulitayarishwa kwa ajili yenu tangu mwanzo wa ulimwengu, aleluya.

MAOMBI
Tumshukuru Mfalme wa wafiadini, maana huu ndio wakati ambapo alijitoa mwenyewe awe chakula na kinywaji katika Karamu ya Mwisho, na ni wakati ambapo aliutoa uhai wake msalabani.
W. Tunakusifu, ewe Kristo Bwana.

Tunakusifu, ewe Kristo Mwokozi wetu, mfano na nguvu ya wafiadini, kwa kuwa umetupenda mpaka mwisho;- (W.)

Kwa kuwa umewaahidia zawadi ya uzima wa milele wakosefu wanaotubu,- (W.)

Kwa kuwa umeliagiza Kanisa kutolea damu ya agano jipya na la milele, damu iliyomwagika kwa ajili ya maondoleo ya dhambi,- (W.)

Kwa kuwa umetudumisha mpaka siku ya leo huku tukiwa na imani thabiti, imani uliyotujalia,- (W.)

Kwa kuwa ndugu wengi leo wameshiriki kifo chako kiletacho wokovu,- (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, umeifanya damu ya wafiadini izae Wakristo. Kwa mapendo yako, ulijalie Kanisa lako shamba ambalo lilimwagiliwa damu ya Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake likupatie daima mavuno mengi. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.