MTAKATIFU MATIA MTUME
MASOMO
SOMO: Mdo.1:15-17,20-26
Siku zile Petro alisimama kati ya ndugu zake (jumala ya majina ilipata mia na ishirini), akasema,
Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi. katika
habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu, kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi,
akapata sehemu ya huduma hii. Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, Kikao chake na kiwe
ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; tena, Usimamizi wake autwae mwingine. Basi katika watu
waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo
wa Yohane, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka
kwake pamoja nasi. Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na
Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuoneshe ni nani
uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda,
aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa
kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.113:1-8(K)8
Aleluya.
1. Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
Lisifuni jina la Bwana.
Jina la Bwana lihimidiwe
Tangu leo na hata milele.
(K) Amketishe pamoja na wakuu,
pamoja na wakuu wa watu wake.
Au:
Aleluya.
2. Toka maawio ya jua hata machweo yake
Jina la Bwana husifiwa.
Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K)
3. Ni nani aliye mfano wa Bwana,
Mungu wetu aketiye juu;
Anyenyekeaye kutazama,
Mbinguni na duniani? (K)
4. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Na kumpandisha maskini kutoka jaani.
Amketishe pamoja na wakuu,
Pamoja na wakuu wa watu wake. (K)
SHANGILIO: Yn.15:16
Aleluya, aleluya!
Ni mimi niliyewachagua ninyi,
nikawaweka mwende mkazae matunda,
na matunda yenu yapate kukaa.
Aleluya!
INJILI: Yn.15:9-17
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi,
kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi
nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha
yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda
ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui
atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu
nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende
mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu
awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.
MAOMBI
Ndugu zangu wapendwa, Kwa maombezi ya Mitume tumwombe Kristo, Bwana wa Kanisa lake.
1. Uliwaweka mitume kuwa mashahidi wa ufufuko wako na kuwatuma duniani kote waitangaze habari
hii ya furaha: Uwasaidie Baba Mtakatifu J. na maaskofu wote uliowachagua
kuwa mahalifa wa mitumne wako kuliongoza kanisa lako kwa busara na hekima.
2. Uliwaagiza mitume watangaze neno lako kati ya mataifa yote: Uwajaze Roho Mtakatifu wahubiri
wote wa neno lako.
3. Uliweka kanisa lako juu ya msingi wa mitume: Ulifanye Kanisa lako kuwa alama ya umoja na ya
amani kati ya mataifa.
4. Uliwaagiza mitume wawaondolee dhambi wale wote wanaotubu: Uwatie moyo mpya wote wanaoungama
dhambi zao.
Bwana Yesu, unastahili kupokea heshima yote, upokee shukrani na sifa katika Kanisa lako pamoja
na Baba na Roho Mtakatifu sasa na siku zote daima na milele. Amina.